BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda.
TAJIRI wa TP Mazembe Moise Katumbi Chapwe ameona isiwe tabu, kama noma na iwe noma tu. Kabeba 'jeshi' lake na kwenda kulificha nchini Morocco huku mipango kabambe ikisukwa ili kuanza vema katika mechi ya kwanza ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya USM Alger itakayochezwa kwenye dimba la Omar-Hamad nchini Algeria.

Matajiri hao wa Jiji la Lubumbashi wataumana na USMA katika fainali hiyo ngumu na ya kuvutia baada ya kufanikiwa kuiondoa El Merreikh ya Sudan kwa jumla ya mabao 4-2. Mechi ya kwanza ya fainali itachezwa Jumamosi ya wiki hii na kurudiana Novemba 8 jijini Lubumbashi, Uwanja wa TP Mazembe.

Moise Katumbi

Mazembe ilitua Morocco juzi Jumapili ikitokea DR Congo, imeweka kambi yake ya siku tano katika hotel ya Golf ambayo ni ya  kifahari yenye hadhi ya nyota tano iliyopo jijini Marrakech ambapo wanatarajia kuondoka keshokutwa Alhamisi usiku   kuwafuata waarabu hao.

Mazembe inayofundishwa na kocha mfaransa Patrice Carteron inaingia katika fainali hiyo ikiwa ni fainali yake ya saba huku ikiwa imeshinda mara nne. Zamalek ya Misri ndiyo inayoongoza kutwaa kombe hilo mara nyingi ikiwa imebeba mara tano.


Safu ya ushambuliaji ya Mazembe inaongozwa na mastraika wa kutumainiwa wa timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu huku pia ikijivunia uzoefu na vipaji vya nyota kadhaa wa kikosi hicho akiwemo kipa Robert Kidiaba, mlinzi Jean Kasusula, viungo Given Singuluma na Solomon Asante pamoja na washambuliaji Roger Assale na Rainford Kalaba.

Endapo Mazembe itatwaa taji hilo msimu huu basi mastraika Samatta na Ulimwengu wataweka rekodi ya kuwa watanzania wa kwanza kutwaa taji hilo.

BOIPLUS itaendelea kukupa taarifa juu ya kila kinachoendelea kuhusiana na fainali hiyo.

Post a Comment

 
Top