BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally
MABINGWA wa Kombe la Kagame, Azam Fc leo wameidhabu JKT Ruvu bao 4-2 katika mwendelezo wa mechi za Ligi Kuu Bara ambayo imechezwa Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam. Kwa matokeo hayo Azam imepanda kileleni ikiwa na pointi 22 huku Yanga wakiwa na pointi 20.

Mabao ya haraka haraka yaliyofungwa na washambuliaji wa Azam, Didier Kavumbagu katika dakika ya nne na John Bocco aliyefunga dakika ya sita tu tangu mchezo huo uanze yaliwachanganya Maafande hao ambao wanashika mkia kwenye msimamo wa ligi hiyo.


Didier Kavumbaghu


Kavumbagu alifunga bao hilo akimalizia mpira uliopigwa na Michael Bolou wakati Bocco akifunga bao hilo ambalo lilitokana na krosi ya Kavumbagu.


Dakika ya 31, Najim Malugu aliifungia timu yake ya JKT Ruvu akipokea pasi ya Saady Kipanga ambaye alipiga mpira wa faulo na kuwababatiza wachezaji wa Azam ambao waliurudisha ndani na kumfikia Kipanga aliyempa Malugu na kupiga shuti lililomshinda kipa wa Aishi Manula.


JKT nusura wapate bao la pili baada ya Kipanga kupiga shuti ambalo Manula lilimtoka na mchezaji wa Azam kuoka na kulitoa nje ikiwa ni dakika ya 36 ambapo lango la Azam liliendelea kushambuliwa ingawa JKT hawakuwa na bahati ya kufunga.


Kipindi cha pili makocha wa timu zote 

mbili walifanya mabadiliko ambapo kocha wa Azam, Stewart Hall alimtoa Michael Bolou, Farid Musa na John Bocco huku akiwaingiza Himid Mao, Erasto Nyoni na Kipre Tchetche wakati Abdallah Kibaden aliwatoa Gaudence Mwaikimba, Saady Kipanga, Magulu nafasi zao zilichukuliwa na Samuel Kamuntu,  Emmanuel Pius na Abdulrahiman Musa.

Mabadiliko aliyoyafanya Kibadeni yalianzaa matunfa baada ya Pius aliyetokea benchi kuifungia bao la pili ikiwa ni dakika ya 70. Bao hilo lilisababishwa na kona iliyopigwa na Michael Aidan ambapo mpira ulirudi ndani na kumpata Pius aliyefunga kwa mguu.


JKT walikosa bao la wazi dakika ya 62 wakati tayari mabeki wa Azam wakiwa wamepoteana huku wao wakiwa wawili na kipa wa Azam na  baadaye kuokoa mpira huo. Dakika ya 63 mchezaji wa JKT Ruvu, Hamis Shango alimkwatua Shomari Kapombe katika eneo la hatari na hivyo mwamuzi Israel Nkongo kutoa penalti iliyopigwa na Bocco dakika 64 na kuipatia timu hiyo bao la tatu.


Kiungo wa Azam, Salum Abubakar 'Sure Boy' alipewa kadi ya njank baada ya kumchezea rafu Michael Aidan huku mchezaji wa JKT, Musa naye akizawadiwa kadi ya njao baada ya kuonyesha kubishana na mwamuzi, kadi nyingine ilikwenda kwa Agrey Morris baada ya kocha Hall kumpokonya mpira Morris aliokuwa anatakiwa kuurusha.


Azam ilipata bao la nne dakika za nyongeza kupitia kwa mshambuliaji wao Kipre ambaye alianza kuukokota mpira kuanzia kati na kwenda nao pembeni na kupiga shuti lililoingia golini.


Katika mechi nyingine iliyochezwa jijini Mbeya kwenye Uwanja wa Sokoine, Prisons imeifunga African Sports bao 1-0. Bao la Prisons limefungwa na Mohammed Mkopi dakika ya 36.


Post a Comment

 
Top