BOIPLUS SPORTS BLOG

KUNA uwezekano mkubwa wa Kocha Mkuu wa Mbeya City, Juma Mwambusi akatua Yanga kuchukuwa mikoba ya Boniface Mkwasa ambaye ameula kwenye kikosi cha Taifa Stars, mazungumzo kati ya Yanga na Mwambusi yamefikia pazuri.

Mwambusi alitua jijini juzi ambapo jana alishuhudia mechi ya Taifa Stars na Malawi ambayo ni ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2018, Stars ilishinda bao 2-0 mabao hayo yakifungwa na Mbwana Samatta pamoja na Thomas Ulimwengu, wote wanachezea TP Mazembe.

Imeelezwa kuwa baada ya mechi hiyo, Mwambusi alikutana na viongozi wa Yanga akiwemo kocha mkuu, Hans Pluijm kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali ikiwemo makubaliano ya kumpa mkataba huo ambao unadaiwa kuwa Mwambusi ameridhishwa nao na yuko tayari kuachana na Mbeya City.

Baada ya makubaliano hayo, Mwambusi amerejea leo asubuhi jijini Mbeya ambako timu yake inajiandaa na mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba itakayochezwa Oktoba 17, Uwanja wa Sokoine na huenda ndiyo itakuwa mechi yake ya mwisho kuwa na City.

Habari kutoka ndani ya Yanga zinasema kuwa leo kulikuwa na vikao ambavyo viliendelea kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali ikiwemo suala la mkataba huo kutokana na mapendekezo ambayo Mwambusi ameyataka.

"Mwambusi ni kocha mzuri, ni mtaalamu mzuri wa mazoezi ya utimamu wa mwili na yupo makini na kazi yake, Pluijm alipendekeza kuwa na kocha msaidizi kutoka hapa hapa nchini lakini awe mchapakazi, mapendekezo yalikuwa kati ya makocha watatu, Mwambusi, Felix Minziro na Mbwana Makata," alisema kiongozi huyo.

Endapo dili la Mwambusi likikamilika ni wazi kwamba Mbeya City ambayo inaonekana kuwa katika kipindi cha kujijenga upya baada ya kuondokewa na wachezaji nyota zaidi ya 10 kuanza kazi ya kumsaka kocha mkuu atakayemrithi Mwambusi na mwenye uvumilivu kama huyo kutokana na mwenendo mbovu wa timu hiyo.

Yanga iliwahi kumsainisha kiungo wa Mbeya City, Deus Kaseke ambaye alikuwa ni tegemeo la timu hiyo na hivi karibu TFF imemfungia miaka miwili beki wao Juma Nyosso kwa kumfanyia kutendo cha udhalilishaji straika wa Azam, John Bocco hivyo City inaendelea kukosa makali yake.

Post a Comment

 
Top