BOIPLUS SPORTS BLOG

MSHAMBULIAJI wa TP Mazembe na Taifa Stars, Mbwana Samatta yupo katika kinyang'anyiro cha wachezaji wanaowania kiatu cha dhahabu kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika inayoandaliwa na Caf akiwa na mabao sita huku akiweka nia ya kuongeza mabao mawili tu ili atwae kiatu hicho.

Samatta yupo nyuma kwa bao moja dhidi ya Bakri Al-Madina wa timu ya Al-Merreikh ambaye amefikisha mabao saba ingawa tayari timu yake imeondolewa kwenye michuano hiyo na Mazembe ambayo ilishinda mabao 3-0 huku Samatta akitupia mawili.

Mpinzani mwingine wa Samatta ni Mouhcine Lajour wa timu ya Moghreb Tetouan na Roger Assale wa Mazembe ambao pia wana mabao sita kila mmoja.

Samatta ameiambia BOIPLUS kuwa ''Nimejiwekea malengo ya kuongeza mabao mawili ili nitwae kiatu hicho, mabao ambayo yatapatikana kwenye mechi zetu zijazo,''.

Kwa ushindi huo Mazembe itacheza fainali za michuano hiyo na USM Alger ya Algeria.

Samatta na Thomas Ulimwengu wanatarajia kutua nchini usiku wa leo kujiunga na Taifa Stars inayojiandaa kucheza na Malawi mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia.

Post a Comment

 
Top