BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda.
LEO ni siku ambayo watanzania wamefanya maamuzi mazito kwa mustakabali wa taifa hili kwa kumchagua Rais, wabunge na madiwani. Ni jambo la kufurahisha kwamba zoezi hilo limekamilika vizuri na hadi kufikia muda wa vituo kufungwa hakukuripotiwa uvunjifu wowote wa amani licha ya kasoro chache zilizojitokeza. 

Mita 400 za kutoka nyumbani hadi kituo cha kupigia kura zilitosha kuwakumbuka wachezaji walioachwa ama kuondoka Simba ndani ya kipindi cha miaka miwili iliyopita, wachezaji hao wanaweza kuunda kikosi kikali kinachoweza kushinda taji la Ligi Kuu ya Vodacom. Hiki ni kikosi cha Simba kinachoweza kutwaa ubingwa huo.


1. IVO MAPUNDA
Mlinda mlango huyu wa zamani wa Yanga, Taifa Stars, Gor Mahia na Simba aliyoachana nayo kabla msimu huu wa ligi kuanza ana uzoefu mkubwa.  Na kitaalamu uzoefu kwa kipa ni jambo muhimu kwavile inaaminika kuwa uwezo wa kipa huongezeka kadiri anavyozidi kukaa langoni. Ivo bado ana uwezo wa kucheza timu yoyote ya Ligi Kuu na bado akafanya vizuri. Hapa anaingia katika kikosi cha kwanza bila hofu yoyote.

2. SAID NASSOR 'CHOLLO'
Chollo aliwahi kuwa nahodha wa timu hiyo kabla ya aliyekuwa kocha wa Simba, Patrick Phiri kumpa mikoba hiyo Joseph Owino na Hassan Isihaka.

Chollo ana sifa kuu moja ya kujituma. Mara zote timu ilipokuwa ikifanya mazoezi huku wachezaji wakitokea majumbani kwao basi huwezi kumuona yeye akifika mazoezini au kuondoka kwa gari. Mara zote hukimbia 'mdogo mdogo' ikiwa ni kama ziada ya mazoezi yake. Majeruhi yalimwangusha lakini sasa ni beki tegemeo ndani ya kikosi cha Mfaransa Patrick Leiwig wa Stand United. Katika kikosi chake anacheza kwa umakini na uwezo mkubwa  kwenye safu yake ya beki wa kulia.

3. ISSA RASHID 'BABA UBAYA'
Miaka mitatu iliyopita hakuna ambaye alikuwa akihoji kiwango cha Baba Ubaya. Baba Ubaya yule aliyetisha na kikosi cha Mtibwa Sugar ya Morogoro hadi kuwafanya mabosi wa Simba watokwe na udenda na kuamua kumpa mkataba mzuri, ilikuaje akashindwa kung'aa akiwa na wekundu hao?. Jibu la swali hili laweza kuwa mtihani mwingine. Kwasasa Baba Ubaya amerudi Mtibwa na moja kwa moja kujihakikishia namba katika kikosi cha kwanza. 

Tangu Mohamed Hussein 'Tshabalala' aliposajiliwa Simba ndio ulikuwa mwanzo wa kiwango cha Baba Ubaya kuanza kushuka. Mbaya zaidi kabla ya kuanza kwa msimu uliopita aliumia nyama za paja ambazo zilimuondoka kabisa kwenye kikosi cha kwanza cha Simba. Msimu mzima uliopita Baba Ubaya amecheza dakika zisizozidi 40 kwa mechi alizoingia.

4. JORAM MGEVEKE
Huyu ni kinda ambaye ni zao la programu ya Taifa Stars Maboresho. Ana nguvu na umbo halisi la mlinzi wa kati, uwezo mkubwa wa kukaba na 'roho mbaya' ya kupambana na washambuliaji wasumbufu. Inawezekana  Simba walitarajia matunda ya haraka tu ndio maana walimuona si kitu na kuamua kumpeleka kwa mkopo Mwadui Fc. Ila kama wangevuta subra basi  angekuwa msaada hapo baadae. 

Msimu huu beki huyo aliomba aachwe huru alisajiliwe moja kwa moja na Mwadui jambo ambalo viongozi wa Simba lilikuwa gumu kulitelekeza hata hivyo Mgeveke ambaye anafanya vizuri katika kikosi hicho kinachofundishwa na Jamhuri Kihwelo 'Julio' mkataba wake unaenda ukingoni.

5. JOSEPH OWINO
Mkongwe ambaye aliwahi kuvaa beji ya unahodha kwa muda mrefu kutokana na sifa zile zile alizokuwa nazo Chollo aliyemuachia unahodha huo. Owino ni moja kati ya wachezaji ambao watacheza mpira kwa kipindi kirefu sana kutokana na nidhamu yao ndani na nje ya uwanja. 


Beki huyu kisiki alikuwa ni tegemeo ndani ya Simba lakini katika hali ya kustaajabisha hakuongezewa mkataba pindi ulipomalizika. Owino anaweza kuwa msaada mkubwa ndani ya kikosi chochote kinachoshiriki Ligi Kuu kwasasa, ikiwemo Simba yenyewe iliyomuacha.

6. PIERRE KWIZERA
Aliingia Simba kipindi ambacho kiungo tegemeo na kipenzi cha wanasimba, Jonas Mkude alikuwa majeruhi. Katika mechi yake ya kwanza tu mashabiki wa wekundu hao walikaa vikundi vikundi na kuanza kujadili juu ya hatma ya Mkude wakiamini hawezi kurudi akaweza kumkalisha benchi Mrundi huyo.
Unajua kilichotokea?, Ujio wa Mkude tena akiwa hajawa fiti vizuri ndo ulikuwa mwisho wa Kwizera kutamba na kikosi cha kwanza cha Simba, maisha yalibadilika na akaanza kukalia benchi hadi alipoachwa rasmi. Kwizera alipotoka Simba alikwenda  kucheza soka nchini Rwanda lakini bado ana uwezo mkubwa wa kucheza ligi hapa nchini.

7. EMMANUEL OKWI
Hii ndo ilikuwa roho ya Wanasimba, wenyewe humuita 'Mtoa roho' wakimaanisha mtu anayeweza kuiangamiza timu pinzani dakika yoyote na bila mandalizi ya muda mrefu. Siku zote Okwi amekuwa shujaa wa Simba na hata sasa ikitangazwa anatua Uwanja wa Ndege kuja kuichezea Simba basi ndani ya dakika chache  mashabiki watajaa kumpokea. Okwi aliondoka Simba na kujiunga na klabu ya Sonderjske inayoshiriki ligi ya Denmark (Danis Superliga) kwa ada ya uhamisho ya Sh 220 milioni.
Okwi anakuwa huru zaidi akipewa jukumu la kushambulia kutokea  upande wa kulia.
8. ABDALLAH SESEME
Huyu ni mmoja kati ya vijana waliokulia katika kikosi cha vijana cha Simba  na kutabiriwa kuja kuwa nyota ndani ya kikosi hicho cha Wekundu wa Msimbazi. Licha ya uwezo mkubwa waliounyesha na kupata mafanikio ikiwemo kubeba kombe la BancABC Super 8, bado mfumo uliwatoa kwenye reli vijana hao na sasa Seseme amekabidhiwa dimba pale Toto Africans jijini Mwanza. Seseme mwenye uwezo mkubwa wa 'kuuficha' mpira bado ana nafasi kubwa ya kufanya vizuri na kufufua ndoto zake kwavile bado ana umri mdogo tu. Seseme ni mtaalamu pia wa kupiga pasi za mwisho.

9. AMISSI TAMBWE
Unaweza kumuita 'Silent Killer' kwa maana ya muuaji wa kimya kimya. Tambwe ni mmoja kati ya viashiria vya makosa makubwa ya kiufundi yaliyofanywa na Simba. Kumuacha Tambwe ilikuwa ni sawa na kuweka bastola chini ili ujaribu kutumia kisu kupambana na adui. Hakuna sababu ya kuweka maneno mengi hapa, Tambwe mwenyewe anatumia miguu na kichwa chake kuthibitisha haya, hadi sasa ni mfungaji tegemeo ndani ya Yanga huku akiwa anaongoza kwa kutoa pasi za mabao kwa washambuliaji wenzake. Kwenye kikosi cha Waliokatwa Fc atasimama kama mshambuliaji wa kati na kwa pasi za Seseme na krosi za Okwi na Singano angeibuka Mfungaji
Bora.

10. SHABAN KISIGA 'MARLONE"
Jamaa anazeeka na utamu wake, vijana wa mjini hapa wanasema 'jua linazama na makali yake'. Kisiga ni mkongwe ambaye kama ataendeleza nidhamu na kuheshimu kazi yake basi anaweza kuendelea kubaki uwanjani kwa miaka kadhaa mbele. Kwasasa anakipiga na kikosi cha Ruvu Shooting inayoshiriki ligi daraja la kwanza (FDL). Aliondoka Simba ghafla bila taarifa yoyote ingawa baadae aliwaambia wanahabari kuwa amechoshwa na maamuzi mabovu ya viongozi wa Simba.


11. RAMADHAN SINGANO 'MESSI'
Kwa Simba hii ya sasa, kama kuna shabiki atasema hamuhitaji Singano au mchezaji wa aina ya Singano ndani ya Simba basi ni lazima uamini kuwa mpira una mambo mengi. 

Ni wazi kuwa Singano aliondoka Simba na kujiunga na Azam akiwa bado anahitajika kwa kiwango kikubwa na Simba, hii ndio sababu hadi leo bado viongozi wa Simba wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili Zacharia Hans Poppe, wanaendelea kulalamikia hukumu iliyotolewa na TFF iliyomtangaza Singano kuwa mchezaji huru. Kwasasa hapati nafasi mara kwa mara katika kikosi cha kwanza cha Azam ila katika mchezo wa ligi dhidi ya Yanga uliochezwa Jumamosi iliyopita aliuthibitishia umma kuwa bado yeye ni moto mkali. Kwenye kikosi hiki anapewa jukumu la kushambulia akitokea upande wa kushoto.

WACHEZAJI WA AKIBA
Kikosi hiki kinaweza kushiriki Ligi Kuu ya Vodacom na kikachukua ubingwa au kushika nafasi ya pili kwavile licha ya kuwa na kikosi cha kwanza imara na chenye vipaji vya hali ya juu, bado kuna wachezaji wa akiba ambao ni hatari na wenye uwezo wa kubadili matokeo muda wowote.

Kwenye benchi kutakuwa na kipa kinda Abuu Hashim, kiraka Willium Lucian 'Gallas' ambaye yupo Ndanda kwa sasa, huyu ana uwezo mkubwa kucheza kama mlinzi wa kulia au kiungo mkabaji.
Benchi pia atakuwepo straika wa Stand United anayeongoza kwa mabao kwenye ligi Elius Maguli ambaye hadi sasa ana mabao manane sawa na mabao yote yaliyofungwa na timu ya Simba msimu huu. Maguli na uongozi wa Simba walikubaliana kwa pamoja kuvunja mkataba wa mchezaji huyo ili awe huru baada ya kocha wa Simba Dylan Kerr kusema hamuhitaji.

Kwenye wachezaji wa akiba pia atakuwepo Danny Sserunkuma ambaye nae alivunja mkataba na Simba kwa makubaliano ya pamoja na uongozi baada ya Simba kutoridhishwa na uwezo wake.

KOCHA
Simba imebadili makocha kadhaa katika kipindi cha miaka miwili lakini ambaye ataendelea kukumbukwa na mashabiki kwa mpira mzuri ni Goran Kopunovic ambaye anakabidhiwa kikosi hiki.

Kama una maoni juu ya kikosi hiki wasiliana na mwandishi wa makala hii kwa namba 0788334467 
Au barua pepe: boiplus.blogspot@boi.co.tz

Post a Comment

 
Top