BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda
FRIENDS Rangers 'Chama la Wana' leo imethibitisha kuwa kweli wamepania kutinga Ligi Kuu Bara msimu ujao baada ya kuibamiza CDA ya Dodoma 'Watoto wa Nyumbani' mabao 2-0, mechi hiyo ya Ligi Daraja la Kwanza ilipigwa katika dimba la Jamhuri mkoani Dodoma.

Friends yenye wachezaji wazoefu kama Steven Mwasyika, Mohamed Banka, Yusuf Mgwao na Amir Maftah ilijipatia bao lake la kwanza dakika ya 38 kupitia kwa mlinzi wake Boniface Nyagawa akimalizia kwa kichwa mpira wa kona iliyochongwa na Mtoro Bofu.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku timu hizo zikishambuliana kwa zamu, lakini bado milango ilikuwa migumu huku mabeki wa timu hizo wakifanya kazi za ziada kuondosha hatari zote.Mabadiliko yaliyofanywa na kocha wa Friends Ally Yusuf 'Tigana' dakika ya 80 ya kuwatoa winga Mgwao na straika Eliuta Mpepo 'Demba Ba' nafasi zao zikichukuliwa na kinda Cliff Buyoya na Joseph John, yalizaa matunda kwani  dakika ya 86, Cliff ambaye anasifika kwa kasi awapo na mpira aliwapunguza mabeki watatu wa CDA na kutoa pasi kwa Joseph ambaye aliipatia Friends bao la pili kwa shuti kali.

Friends wanaongoza ligi hiyo wakiwa na pointi 11 wakifuatiwa na Ashanti United yenye pointi 11 pia ila ikizidiwa kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa. African Lyon inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 10 huku Kiluvya United ikiwa nafasi ya nne na pointi zake tisa.

Post a Comment

 
Top