BOIPLUS SPORTS BLOG

TIMU ya Friends Rangers 'Chama la Wana' ya jijini Dar Es Salaam leo imeibuka na ushindi wa bao 1-0  dhidi ya Polisi Dodoma katika mchezo wa ligi daraja la kwanza FDL . Mechi hiyo ilichezwa kwenye uwanja wa Karume jijini Dar Es Salaam.
Friends inayofundishwa na nyota wa zamani Ally Yusuf 'Tigana' ilipata bao lake pekee katika dakika ya 24 ya mchezo likiwekwa kimiani na straika Eliuta Justine 'Demba Ba' kwa shuti kali la mguu wa kushoto likimuacha kipa wa Polisi Gerald Mwingira akiwa  hana la kufanya.

Straika Eliuta Justine akishangia bao lake 

Baada ya bao hilo Polisi iliongeza mashambulizi huku washambuliaji wake wakijaribu kutafuta bao la kusawazisha lakini uimara wa mlinda mlango Alphonce Raphael wa Friends ulikuwa kikwazo.
Kipindi cha pili Friends ilifanya mabadiliko kwa kuwaingiza winga Cliff Buyoya na mkongwe Mohamed Banka waliochukua nafasi za Yusuf Mgwao na Eliuta.

Winga wa Friends Cliff Buyoya(kulia) akiingia kuchukua nafasi ya Yusuf Mgwao (kushoto)

Kwa matokeo haya Friends inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi saba sawa na Kinondoni Municipal Council (KMC). Kiluvya United inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi nane huku Ashanti ikikamata nafasi ya nne na pointi zake sita mkononi.
Hivi karibuni FDL itaanza kuonyeshwa moja kwa moja na luninga ya Star Tv.

Post a Comment

 
Top