BOIPLUS SPORTS BLOG

MSHAMBULIAJI wa Simba, Hamis Kiiza ameibuka mchezaji bora wa timu ya Simba na kumpiku beki Hassan Kessy baada ya kupata kura zaidi ya 400 zilizopigwa na mashabiki wa klabu hiyo kwa mwezi Septemba.

Kiiza amekabidhiwa tuzo hiyo leo wakati wa mazoezi ya timu hiyo yanayofanyika Uwanja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, tuzo ambayo iliambatana na zawadi ya fedha ya Sh 500,000 pamoja na picha ya kikosi cha timu hiyo.

Viongozi wa Simba waliamua kuanzisha utaratibu wa kutoa tuzo hiyo ili kuwahamasisha wachezaji wao kujituma katika msimu huu wa Ligi Kuu Bara ikiwa ni pamoja na kuleta ushindani.

Kiiza alikabidhiwa tuzo hiyo na kocha wake Dylan Kerr ambaye alimpongeza na kumtaka aongeze juhudi na kwamba tuzo hiyo itawasaidia wachezaji wengine kujituma zaidi.

Kwa upande wa Kiiza ambaye kwa sasa ni majeruhi alisema kuwa ''Nafurahi kuwa mchezaji bora wa Septemba naamini kwa ushirikiano na wenzangu tutaendelea kufanya vizuri kwenye ligi,''.


Post a Comment

 
Top