BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda, aliyekuwa Mbeya.

HAKUNA asiyemfahamu kipa Juma Kaseja katika soka la Tanzania, hata kama hujawahi kumuona kwenye kazi yake basi ni lazima utakuwa umelisikia jina lake hasa kwa wale wanaopenda na kufuatilia michezo.
Kaseja akifurahia jambo na mwandishi wa makala hiiKaseja ambaye amewahi kuzidakia timu za Moro United, Simba, Yanga na Taifa Stars mpaka akapachikwa jina la Tanzania One kutokana na umahiri wake anapokuwa golini kwasasa anaidakia timu ya Mbeya City ya jijini Mbeya.

Mengi Kaseja ameyafanya akiwa Simba, akiwa Yanga na hata Taifa Stars ambayo aliachana nayo ikiwa chini ya kocha Mbrazil, Marcio Maximo na bado klabu ya Simba  wanatamani kuwa naye tena. 

Kaseja mwenye misimamo aliondoka Yanga kwani hakuweza kuvumilia kukaa benchi huku akiamini kwamba kama mchezaji unapaswa upate nafasi ya kucheza.

Hilo tu ndilo jambo pekee ambalo Kaseja anaweza kupongezwa kwani ana misimamo ya kipee na hupenda kuona kiwango chake hakishuki hata kama wengine wanamuona ana umri mkubwa. Kama kawaida maisha ya binadamu yanatofautina kuna wengine wanamuona Kaseja hafai na wengine bado wanahitaji huduma yake.

Katika timu hiyo hajasaini mkataba wa muda mrefu, ana mkataba wa muda mfupi tu na hiyo ni kutokana na makubaliano yao kati yake na viongozi wa Mbeya City. Amedaka mechi saba ambazo timu hiyo imecheza huku ikishika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi nne tu, ikishinda mechi moja ikitoka sare moja na nyingine ikifungwa.

Katika mahojiano na BOIPLUS yaliyofanyika jijini Mbeya, Kaseja alielezea mambo mbalimbali katika soka hasa alipotua Mbeya City ambapo anaelezea kuwa wengi walihisi hawezi kuishi maisha ya jijini humo na huku ikitajwa kuwa ndiyo sababu hata ya kukubaliana kumpa mkataba mfupi.
"Maisha ya Mbeya City ni sawa tu na maisha ya sehemu nyingine, najua wengi walifikiri siwezi kuishi huku ila mimi ni mchezaji ambaye popote naweza kuishi, nilianza kucheza Moro United ambayo ni timu ya mkoani kabla sijaenda Dar es Salaam hivyo hilo si tatizo kwangu," alisema 

Hata hivyo kipa huyo ameonyeshwa kutofurahishwa na matokeo wanayopata kwasasa ingawa anaamini kwamba matokeo hayo yatabadilika hapo baadaye. 

"Unajua Mbeya City ni timu nzuri na ina wachezaji wazuri ndiyo maana hata ukiangalia mechi tulizocheza zote tumecheza vizuri lakini tunafungwa mabao ya ajabu tu, huwa sielewi huwa tunafungwaje, mabao tunayofungwa kwa hakika yanaumiza maana mpira tunacheza vizuri lakini ni kwanini tunafungwa mabao rahisi. 


"Bado naamini kwamba City itafanya vizuri katika mechi zijazo ambazo mbili tunacheza nyumbani, tunalazimika kucheza na kuhakikisha tunashinda, City ni timu nzuri na ina wachezaji wenye vipaji," alisema Kaseja 


Kaseja si tu kwamba anadaka ama kafundishwa kudaka bali ana kipaji hicho ila ameongezewa ujuzi na wengine, na ndiyo maana hata yeye aliamua kwenda kusomea jinsi ya kuwafundisha wengine wajue namna gani ya kusimama golini na kudaka kwa umahiri.  

Kwasasa Kaseja pia ni kocha wa makipa ingawa bado hajastaafu soka na bado ana safari ndefu tu kwenye soka kwani bado hajakutana na changamoto mpya kutoka kwa wachezaji ama makipa wengine wanaochipukia. 

"Mpira hauna uzee, wengi wanasema mimi ni mkubwa lakini je nani yupo wa kunipa changamoto?. Wengi katika soka wanavunjika mioyo ya kuendelea kucheza kwasababu tu wanakatishwa tamaa na watu wengine, ningekuwa mtu wa kukata tamaa basi ningekuwa nimestaafu soka miaka mingi, mengi yamesemwa juu yangu lakini huwa siyafuatilii najua ninachokifanya," anasema. 


Wakati anatua Mbeya City, Kaseja alipokelewa na kocha Juma Mwambusi ambaye kwasasa ni kocha msaidizi wa Hans Pluijm wa Yanga, Kaseja anasema ni vigumu kwake kumuelezea zaidi Mwambusi kwani hajakaa naye muda mrefu. 


"Kila kocha ana falsafa yake ya ufundishaji, Mwambusi alikuwa ni kocha mzuri na siwezi kuzungumzia mazuri pekee kwani hakuna binadamu asiyekuwa na kasoro, hivyo kila mtu ana mazuri na mabaya yake, hata huyu Mingange ni mzuri ila lazima naye atakuwa na mapungufu yake," anasema Kaseja.

Wakati yupo Simba, Kaseja alikuwa akicheza pamoja na kiungo Haruna Moshi 'Boban' na sasa wamekutana katika kikosi hicho huku Kaseja akielezea furaha ya ujio wa kiungo huyo.

"Boban bado ni mchezaji mzuri, naamini ataisaidia Mbeya City kwa kiasi kikubwa sana, ingawa kwasasa bado hajazoea hali ya hewa na hajafanya mazoezi na timu muda mrefu, ila bado Boban ana kitu katika soka la Tanzania.

"Na si hilo tu bali pia kuna faida ya Boban kuja Mbeya City kwasasa ambayo ina vijana wengi, naamini kwa uzoefu na umri wake atakuwa mshauri mzuri kwa vijana ndani ya kikosi chetu hiki, maana hii timu ina vijana wengi wanaohitaji kuongozwa," alisema.

Mashabiki wa Mbeya City kwasasa ni kama wamekata tamaa na timu yao kutokana na kufanya vibaya kwenye ligi ukilinganisha na msimu wa kwanza ambao timu hiyo ilipanda daraja na kuzisumbua timu nyingi za ligi kuu hasa Simba, Yanga na Azam.

Kwasasa makali ya Mbeya City hayapo tena na kupoteza mashabiki wengi ambapo hata uwanjani kwa mechi za msimu huu na uliopita walipungua kwa kiasi kikubwa lakini Kaseja amewapa neno mashabiki wa timu hiyo kwakusema kuwa wasikate tamaa.

"Tunawaomba mashabiki kuendelea kutoa ushirikiano mkubwa, wasiingize siasa kwenye soka, mpira ndivyo ulivyo kuna kushinda na kufungwa, hiki kipindi wanapaswa kutoa ushirikiano mkubwa kwani bado tuna nafasi ya kufanya vyema mechi zinajazo na kurudisha heshima ya Mbeya City.

"Mimi nafikiri kama timu ingekuwa inacheza vibaya labda ndiyo wangekata tamaa ila timu inacheza vizuri na ina wachezaji wazuri lakini mabao yanayofungwa ni ya ajabu ajabu tu," anasema.

Kaseja alimaliza kwa kuwaasa wadau wote wa Mbeya City kuendelea kutimiza wajibu wao.
"Wachezaji hatupaswi kukata tamaa, tupambane uwanjani kama kawaida. Mashabiki watupe sapoti  uwanjani na viongozi waendelee na kutupatia mahitaji yetu kama wafanyavyo sasa, naamini tutaanza kupata matokeo mazuri"

Post a Comment

 
Top