BOIPLUS SPORTS BLOG

 KATIKA kile kinachoonekana ni furaha iliyopitiliza kwa timu yake kutinga hatua ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mmiliki wa klabu ya TP Mazembe, Moise Katumbi ametoa zawadi ya dola 800,000 sawa na Sh 1.6 Bilioni kwa wachezaji na benchi la ufundi la timu hiyo.

Tukio hilo lilitokea baada ya mechi kati ya Mazembe na Al Merreikh kumalizika kwa timu hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 na kutinga fainali kwa ushindi wa jumla ya mabao 4-2. Katika mechi ya awali iliyopigwa nchini Sudan, Al Merreikh ilishinda mabao 2-1

Kwenye mitandao ya kijamii jana kulisambaa taarifa kwamba Katumbi ametoa kiasi cha dola 800,000 kwa kila mchezaji kiasi ambacho kilizua mijadala mizito huku wengine wakisema ni kikubwa mno na  kinashtua. Kutokana na hilo BOIPLUS ilimtafuta straika Mbwana Samatta anayekipiga katika klabu hiyo ili atoe ufafanuzi juu ya jambo hilo.

Samatta alikanusha suala la kila mchezaji kupokea kiasi hicho ila alikiri kuwa Katumbi ametoa dola 800,000 ambayo itagawanywa kwa wachezaji 30, makocha watano na mtunza vifaa mmoja katika uwiano unaoendana na mchango wa kila mmoja katika mechi hizo mbili.

"Hizo ni stori tu kaka, pesa aliyotoa tunagawana wachezaji, makocha na mtunza vifaa," alisema Samatta.

Straika huyo ambaye tayari ameshatua nchini akiwa na Thomas Ulimwengu kwa ajili kuisaidia timu yake ya Taifa katika mchezo wao dhidi ya Malawi hapo kesho alikataa katakata kutaja kiasi ambacho yeye binafsi amepokea katika mgao huo.

Post a Comment

 
Top