BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda
STRAIKA wa Azam Fc, Didier Kavumbagu leo ameibuka kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya timu yake na JKT Ruvu na kuonyesha kiwango cha hali ya juu licha ya kuwa alitupwa benchi tangu ligi imeanza.

Tangu kuanza kwa ligi hiyo Kavumbaghu hajawahi kuanza katika kikosi cha kwanza cha Muingereza, Stewart Hall na mara zote alianzia benchi ambapo alikuwa akipewa dakika zisizodi 20.


Katika ushindi wa Azam wa mabao 4-2 dhidi ya JKT Ruvu mechi iliyochezwa Uwanja wa Karume, Kavumbagu alifunga bao moja huku akisababisha bao la pili lililofungwa na John Bocco.

Kavumbagu ameiambia BOIPLUS kuwa anasikitishwa na kitendo cha kukaa benchi wakati kazi yake ni kucheza na kwamba hayupo tayari kuendelea kuwepo kwenye kikosi hicho hasa kipindi hiki cha kuelekea usajili wa dirisha dogo.

''Sipendi kukaa benchi, nipo kwa ajili ya kucheza na kama itashindikana basi nitaondoka kwenda kucheza sehemu nyingine na si hapa pekee nitaenda hata nje ya Tanzania,'' alisema Kavumbagu

Mchezaji huyo ambaye ndiye mfungaji bora wa Azam wa msimu uliopita ambapo alifunga mabao 11 aliwahi kutajwa kujiunga na Simba walioonyesha ni ya kumchukuwa kwa mkopo msimu huu lakini suala lake hilo lilionekana kuwa gumu.


Kavumbagu ambaye alikuwa ni miongoni mwa wachezaji waliokuwa wakiunda kikosi cha timu ya Taifa ya Burundi lakini sasa amepoteza namba kwenye kikosi hicho kutokana na kusugua benchi.

''Inaniuma kwasababu hata kwenye kikosi cha timu yangu ya Taifa simo na siwezi kuitwa kwasababu hapa sipewi nafasi ya kucheza, hivyo ni lazima niwe na msimamo wangu maana hii ndiyo kazi yangu,'' alisema Kavumbagu

Post a Comment

 
Top