BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally, Mbeya.

KOCHA mkuu wa Simba, Dylan Kerr amesema kuwa hajafurahishwa na kiwango cha wachezaji wake walichokionyesha kwenye mechi yao dhidi ya Mbeya City na kwamba sasa atakuwa mkali ili kila mmoja atambue majukumu yake uwanjani.

Katika mechi hiyo iliyochezwa jana Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya, Simba ilipata bao pekee la ushindi kupitia kwa beki wao Juuko Murshid huku wenyeji Mbeya City wakishindwa kuzitumia vizuri nafasi kadhaa walizopata na kuifanya Simba kuondoka na pointi tatu ikiwa ni mara yao ya kwanza tangu waanze kucheza na City ilivyopanda daraja.

Kerr amesema kuwa kuna haja ya kufanyia kazi mapungufu hayo kabla ya kukutana na Prisons Jumatano ijayo katika Uwanja huo huku akisisitiza kwamba lengo lake ni kupata pointi sita kwa mechi zote atakazocheza Uwanja wa Sokoine.

"Nafurahia kupata ushindi huu lakini sijafurahishwa kabisa na kiwango walichokionyeshwa leo, wakati wa mazoezi wanafanya vizuri lakini wakifika uwanjani wanashindwa kufuata yale niliyowaelekeza toka awali na ndiyo maana mechi imekuwa ngumu kwetu.

"Mbeya City ni timu nzuri na wamecheza vizuri ingawa hawakuwa na bahati na kutufunga, nampongeza kipa wangu Angban (Vincent) kwa uwezo aliounyesha leo hakika kacheza vizuri na amesaidia sana ili tusifungwe," alisema Kerr.

Katika mechi hiyo, Kerr alitumia viungo watano lakini walifunikwa na wachezaji wa Mbeya City walioonekana kuumiliki mpira kwa muda mwingi.

Post a Comment

 
Top