BOIPLUS SPORTS BLOG

SIMBA wapo jijini Mbeya na wanajiamini kweli kweli kwamba ni lazima warudi Dar es Salaam wakiwa na pointi sita mkononi ambazo watazipata katika mechi yao ya Jumamosi dhidi ya Mbeya City na ile wiki ijayo watakapocheza na Prisons.

Jeuri hiyo ameitoa kocha wao Dylan Kerr ambaye amesema matokeo yao yatatokana na jinsi alivyouona uwanja wa Sokoine utakaotumiwa katika mechi zao zote mbili kwamba utawapa matokeo mazuri.

Kerr amesema kuwa anajivuni uimara wa kikosi chake lakini bado habweteki na wala hadanganyiki juu ya kuondoka kocha mkuu wa Mbeya City, Juma Mwambusi aliyetua Yanga kwamba waione mechi hiyo ni nyepesi.

"Tumekuja kutafuta pointi sita muhimu hapa Mbeya, nimeuona uwanja tutakaotumia na nimejua jinsi gani ya kuwapanga wachezaji wangu kutokana na uwanja ulivyo, lakini pia sitaki kujisahau kwamba Mbeya City imeondokewa na kocha wao mkuu hivyo ni rahisi kwetu kupita.

"Ninachokifanya ni kujipanga kila idara kuanzia maandalizi mpaka mechi yenyewe, nikimalizana na Mbeya City tutakuwa na kazi nyingine na Prisons ambapo tutakuwa tumekuwa wazoefu zaidi ya hivi sasa. Lengo letu ni kupata ushindi wowote," alisema Kerr.

Tangu jana Simba imekuwa ikifanya mazoezi yake Uwanja wa Sokoine baada ya kocha huyo kuomba kuhama kwenye Uwanja wao wa awali wa Itende jeshini, mazoezi hayo huanza baada ya Mbeya City kumaliza yao hivyo Simba huingia mchana wa jua kali.

Katika mechi hiyo, Kerr atawakosa wachezaji wake Hamisi Kiiza ambaye anasumbuliwa na nyama za paja, Hassan Kessy mwenye kadi tatu za njano, Emiry Nimubona ambaye amevunjika kidole cha mkono na amebaki jijini Dar es Salaam ambapo mbadala wao wanaweza kuwa ni Maganga na Simon Sserunkuma.

Post a Comment

 
Top