BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Christian Simba
KAMATI ya Utendaji ya Shirikisho la Soka la Cameroon (Fecafoot) jana ilimfuta kazi Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Cameroon, Volke Finke.

Finke, 67, ambaye ni raia wa Ujerumani, amekuwa akifundisha timu hiyo tangu Mei, 2013 lakini chini ya uongozi wake, timu hiyo imekuwa ikipata matokeo mabaya hasa katika fainali za Kombe la Dunia 2014 na fainali za Kombe la Taifa Bingwa Afrika 2015.


Fecafoot walitangaza kupitia akaunti yao ya Twitter kwamba Alexandre Belinga ameteuliwa kuongoza timu hiyo ambapo atasaidiwa na Djonkep Bonaventure.

Wawili hao sasa huenda wakawa ndio watakaoiandaa Cameroon kwa mechi mbili za kufuzu Kombe la Dunia 2018 dhidi ya Niger Novemba 13 na 17.

Cameroon walijulikana kwa ubabe wao wa soka Afrika lakini kwa miaka mitano sasa hawana makali hayo baada ya Finke kushindwa kubadilisha mwenendo wa kikosi hicho.

Katika Kombe la Dunia lililofanyika nchini Brazil, timu hiyo chini ya Finke ilishinda mechi zote tatu na baadhi ya wachezaji wake waliadhibiwa kwa utovu wa nidhamu. Alex Song alionyeshwa kadi nyekundu na wenzake Benoit Assou-Ekotto na Benjamin Moukandjo walipigana uwanjani.

Cameroon walionekana kujikwamua kutoka kwa masaibu hayo walipofuzu fainali za Kombe la Taifa Bingwa Afrika nchini Equatorial Guinea bila kushindwa lakini walitolewa hatua ya makundi kwenye fainali hizo.

Post a Comment

 
Top