BOIPLUS SPORTS BLOGSHIRIKISHO la Mpira wa Miguu nchini (TFF) leo limeingia mkataba wa miaka mitatu wenye thamani ya Sh 450 milioni na kituo cha televisheni cha Star Tv kurusha matangazo ya Ligi Daraja la Kwanza nchini (FDL)

Akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa kusaini mkataba huo, Rais wa TFF Jamal Malinzi aliishukuru kampuni ya Sahara Media Group kwa kuamua kuwekeza katika mpira wa miguu nchini kwa kuamua kuonyesha Ligi Daraja la Kwanza.

Malinzi ameziomba klabu za FDL kutumia udhamini huo kama chachu ya mafanikio na kufanya vizuri katika ligi hiyo itakayotoa timu tatu za kupanda Ligi Kuu ya Vodacom msimu ujao.

Malinzi amewaomba wamiliki wa viwanja vinavyotumika kwa michezo ya FDL kuviweka katika hali nzuri ya matunzo ili mechi zinazochezwa katika viwanja hivyo ziweze kuwa nzuri kiufundi na muonekano wa kwenye runinga.

Jumla ya udhamini wa Ligi Daraja la Kwanza kwa sasa Sh 1.35 bilioni ikiwa ni pamoja na udhamini wa Sh 900 milioni  kutoka StarTimes ambaye ni mdhamini mkuu wa FDL na Sh  450 kutoka StarTv.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Sahara Media Group, Samwel Nyala ameishukuru TFF kwa kuwapa nafasi hiyo ya haki za matangazo kampuni yake kwa michezo ya Ligi Daraja la kwanza nchini (FDL).

Katika kuhakikisha michezo hiyo inaonekana kwa wingi zaidi, Nyala alisema watafungua mkondo (Channel) ya Star Sports Plus itakakuwa inaonyesha michezo tu ikiwemo ligi hiyo ya FDL.

Akizungumza kwa niaba ya klabu za FDL, Asha Kigundula ambaye ni Msemaji wa Klabu ya Friends Rangers ya jijini Dar es Salaam, ameishukuru TFF kwa kuweza kuwapatia udhamini kwenye ligi, jambo ambalo litawapelekea kujiandaa na kufanya vizuri katika ligi msimu huu.

Post a Comment

 
Top