BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally, Mbeya.


MGOMBEA Urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) anayeungwa mkono na Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi(UKAWA), Edward Lowassa ameahirisha mkutano wake wa kampeni uliopangwa kufanyika kesho jijini Mbeya na sasa utafanyika keshokutwa Jumapili.

Lowassa ameahirisha mkutano huo na kuifanya mechi ya Simba na Mbeya City ipate mashabiki wengi ambao wengi wao kama kungekuwepo na mkutano huo wangekwenda kumsikiliza mgombea huyo.

Habari zilizopatikana jijini hapa ni kwamba baada ya kuona mechi hiyo inachezwa jijini hapa Lowassa ameamua kuanza kampeni zake wilayani Momba Mbozi na keshokutwa ataanzia Mbarali, Chunya na kumalizia Mbeya Mjini.

Taarifa hiyo imekuwa njema kwa timu zote mbili Simba na Mbeya City ambazo zilikuwa zikihofia kupoteza mashabiki wake na kupoteza asilimia kubwa ya mapato endapo mkutano huo ungefanyika kesho.

Simba ipo jijini Mbeya kwa muda wa wiki moja sasa wakijiandaa na mechi hiyo huku taarifa zaidi zikisema mashabiki wa Mbeya City wengi wao wanamuunga mkono mgombea Ubunge jimbo Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi.

Post a Comment

 
Top