BOIPLUS SPORTS BLOG

JUZI Jumatano  Taifa Stars  iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Malawi 'The Flames' katika mchezo wa awali wa kufuzu michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2018. Mechi hiyo ilichezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mabao ya Stars yaliwekwa kimiani na mastraika wanaoichezea klabu ya TP Mazembe ya Congo, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu. Timu hizo zitarudiana keshokutwa Jumapili jijini Blantye, Malawi.


Ushindi wa Stars katika mchezo wa awali ni ushindi mzuri tu hasa kwavile Flames hawakupata bao lakini ukiutathimini mchezo huo unaweza kugundua kuwa haukutosha na si ushindi wa kujivunia sana.
Zipo sababu kadhaa zinazoweza kuwa zimeifanya Stars kutoibuka na ushindi mnono, kama vile safu ya ushambuliaji kupoteza nafasi kadhaa za wazi nk.
BOIPLUS inaelezea sababu ya msingi iliyoinyima ushindi mnono Stars huku ikitoa tahadhari yake kuelekea mchezo wa marudiano utakaopigwa baada ya takribani masaa 58 tu yajayo.
Jambo jema ni kwamba Kocha Mkuu wa Stars, Boniface Mkwasa amekiri mechi hiyo itakuwa ngumu na ni lazima Stars ijifunge mkanda ili kufanikiwa kuitoa Malawi.
Katika mchezo wa awali Malawi walifanikiwa kwa kiasi kikubwa kutawala eneo la kiungo huku wakitengeneza mashambulizi kadhaa yaliyozaa kona kumi  ambazo hazikuzaa matunda huku Stars ikipata kona tano tu. 

Gerald Phiri akimchunga kwa umakini Ulimwengu


Kiungo Gerald Phiri wa Malawi juzi ni kama vile alikodi eneo la kati la uwanja na kulitumia kuharibu mipango mingi ya Stars kulifikia lango lao huku mara kadhaa akipandisha timu mbele. Ni dhahiri Phiri akishirikiana vema na viungo wengine wawili Chimango Kayira na Micium Mhone walifanikiwa kuwafunika Himid na Ndemla.

Mkwasa akiwaelekeza jambo viungo wake Himid na Ndemla

Hakuna asiyejua uwezo wa hali ya juu wa Himid na Ndemla, lakini ni wazi kuwa kitendo cha Mkwasa kupanga viungo wa katikati wawili tu dhidi ya watatu wa Flames kilikuwa ni sawa na kubeti. Vijana hawa walijitahidi kwa kadiri ya uwezo wao kuunganisha timu lakini changamoto kubwa ilikuwa ni hawa viungo watatu wa Flames. Mkwasa alipanga hivyo timu akiwa amejiandaa kuwashambulia Malawi mwanzo mwisho ili kupata mabao mengi. Hii ndio ilimfanya aweke viungo wawili tu wa kati huku katika mstari wa mbele akijaza nyota wanne wakiwemo Farid Mussa na Ulimwengu waliokuwa wakishambulia kutokea pembeni pia Samatta na Mrisho Ngassa waliokuwa washambuliaji wa kati.

Kitendo cha Flames kufika langoni mwa Stars mara nyingi tena wakipitia katikati ya Uwanja, ni wazi kwamba 'mkeka' wa Mkwasa ulikuwa unaelekea kuchanika, shukrani kwa mabao mawili ya Samatta na Ulimwengu kwa maana ndiyo yaliyofanya mambo yasiharibikie nyumbani.

Telela(kulia) akiwajibika katika eneo la kiungo baada ya kuingia kuongeza nguvu

Kosa hapa lilikuwa ni kusahau kwamba Malawi walijua wanakuja kucheza ugenini hivyo ni lazima walijiimarisha sana katika eneo la ulinzi na kiungo, Mkwasa hakupaswa kupunguza idadi ya viungo wa kati, badala yake angetumia winga mmoja na viungo watatu wa kati.
Kiungo Salum Telela ndiye aliyethibitisha haya kwa maana kuingia kwake kulibadili kila kitu katika eneo la kati la uwanja. Alimpunguzia majukumu Mao kwa kufika kila mpira ulipotua, alikaba, aliharibu mipango yote ya Flames na naamini kama angeanza tangu mwanzo au kuingia mapema basi Stars ingepata ushindi mnono.

Telela aliingia badala ya Ngassa aliyekuwa akicheza kama mshambuliaji pacha wa kati na Samatta lakini yeye alipewa jukumu la kwenda kuongeza nguvu kwenye kiungo.
Alichofanya Telela katika dakika chache alizocheza kilikuwa ni kumuonyesha Mkwasa kuwa  bila kujali kuwa timu ilikuwa nyumbani, bado ilihitaji uimara kwenye kiungo.  Mkwasa hapaswi 'kubeti' tena kwenye mchezo wa marudiano, akifanya hivyo safari ya Stars itaishia Malawi.

Ubora wa Flames umeonekana wazi wazi, si tu kocha Mkwasa bali hata nyota Samatta, Ulimwengu na Nahodha, Nadir Haroub walikiri kuwa ni timu ngumu na wanahitaji kufanya kazi ya ziada kuiondoa mashindanoni licha ya ushindi walioupata nyumbani. Kutokana na hili Mkwasa hana sababu ya kujiuliza mara mbili juu ya kutumia viungo watatu wa kati, BOIPLUS inaamini ameona mapungufu katika mchezo wa awali na atayafanyia kazi.
Himid na Ndemla walicheza vizuri lakini wakiwa Malawi watahimhitaji Telela kuanzia dakika ya kwanza ya mchezo. Kocha  atalazimika kubadili mfumo alioutumia mwanzo wa 4-2-3-1 na kucheza 4-3-3. Hii ina maana kwamba italazimu mmoja kati ya Farid Mussa au Ngassa aanzie benchi ili kupisha nafasi kwa viungo wakabaji wawili na kiungo mshambuliaji mmoja kuwemo uwanjani kwa dakika zote 90.

Kwa kiwango kilichoonyeshwa na Flames  hawapaswi kuachwa watawale eneo la kiungo, lakini pia ukuta wa Stars ukiongozwa na Canavaro unapaswa kuwa makini sana na mshambuliaji wa kati wa Flames, Chawangiwa Kawanda. Ni aina ya washambuliaji wasumbufu wenye kasi na nguvu, hana tofauti na Ulimwengu wa Stars, kwahiyo bila kuwa makini nae kwa kipindi chote cha mchezo, straika huyu anaweza kumaliza safari yetu ya kuelekea Kombe la Dunia pale pale Malawi.


Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu namba 0788334467 au e-mail: karim@boi.co.tz

Post a Comment

 
Top