BOIPLUS SPORTS BLOG

WAKATI dirisha la usajili majira ya baridi likiwa linakaribia kufunguliwa, kila siku tetesi mpya na nzito za usajili zinazidi kupamba moto.

Habari zinazobamba kurasa za magazeti ni kwamba kocha Jose Mourinho yupo kwenye foleni ya kutupiwa virago Chelsea.

Msimu wa adha kwa Chelsea umeendelea Jumanne baada ya klabu hiyo kufungwa na Stoke City katika mechi yao ya Kombe la Capital One kwa mikwaju ya penalti kufuatia sare ya 1-1. Matokeo hayo yameongeza joto kwenye kiti cha Jose Mourinho Stamford Bridge na anaweza kukikosa kibarua chake muda wowote kabla ya sikukuu za Krismasi mwaka huu.


Jina moja ambalo si geni linaloweza kuchukua nafasi ya Bwana Special One ni Carlo Ancelotti. Gazeti la The Daily Telegraph limeripoti kuwa kocha huyo wa zamani wa Real Madrid (na Chelsea) ana nafasi kubwa katika orodha ya watu wanaofikiriwa kwa nafasi hiyo, lakini Muitaliano huyo atarejea klabuni hapo iwapo atapewa mkataba wa kudumu.

Jarida jingine la Daily Mirror limeibuka na kusema Mzee huyo wa miaka 56 atafurahi kurudi tena Darajani iwapo Roman Abramovich atampa mkataba wa kudumu wa muda mrefu.

Mreno ambaye amesaini mkataba mpya wa miaka minne msimu wa majira ya joto, hatakosa kazi kwa muda mrefu kama kibarua chake kitakatishwa Chelsea. Jarida la Independent limesema kuwa Mourinho anaweza kurudi kwenye klabu yake ya zamani Inter Milan au kwenda kufanya kazi kwa mara ya kwanza na Paris Saint-Germain.

Kambi ya Mourinho imeripotiwa kusema kuwa itasisitiza kocha huyo mwenye miaka 52 alipwe mkataba wake wote wa sasa.

Post a Comment

 
Top