BOIPLUS SPORTS BLOG

KOCHA wa Mbeya City, Juma Mwambusi leo asuhubi aliwaaga wachezaji wake katika mazoezi ya kujiandaa na mechi yao ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba itakayochezwa Oktoba 17, Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Mwambusi anahusishwa kujiunga na Yanga kuchukuwa mikoba ya Boniface Mkwasa ambaye sasa amepata ajira ya kuifundisha Taifa Stars.


Tayari mazungumzo ya awali kati ya Mwambusi na viongozi wa Yanga yamefanyika huku ikielezwa kwamba kesho kocha huyo huenda akasaini mkataba na Yanga ikiwa ni pamoja na kuanza kazi.
Endapo Mwambusi akisaini mkataba huo ina maanisha kwamba katika mechi ya City na Simba, Mwambusi hatakuwepo ambapo atakuwa kwenye benchi la Yanga akimsaidia Hans Pluijm kwenye mechi yao na Azam Fc.
Wakizungumza na BOIPLUS kwa masharti ya kutoandikwa majina yao wachezaji hao walisema kuwa City inaendelea kubomoka na hivyo itawalazimu kutumia nguvu nyingi ili iwe imara.
''Ni kweli kocha ametuaga leo asubuhi kuwa hataendelea tena kuifundisha timu yetu, ametusihi tujitume kuhakikisha timu inabaki kwenye ligi, hatuwezi kupinga kwani haya ni maisha ya mtu ila ni pengo kubwa kwenye timu yetu,'' alisema mchezaji huyo.
Katibu Mkuu wa City, Emmanuel Kimbe alipoulizwa juu ya mustakabali wao alisema ''Ndiyo naelekea ofisi nafikiri mpaka jioni tutakuwa tumejua cha kufanya na kutoa kauli yetu,''.

Post a Comment

 
Top