BOIPLUS SPORTS BLOG

SIMBA leo imefanya mauaji kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ikiifunga Majimaji ya Songea bao 6-1 huku Ibrahim Ajibu akidhihirisha uwezo wake wa kufunga akipiga 'hat-trick'.

Tangu ligi ianze Ajibu amekuwa akianzia benchi kutokana na Kocha wake Dylan Kerr kutomwamini huku akidai kiwa hajitumi mazoezini huku mara kadhaa akimtumia Musa Mgosi.


Ajibu alianza kuipatia bao la kwanza timu yake dakika ya nane  akipokea pasi ya Peter Mwalyanzi huku bao la pili akifunga dakika ya 11 ikiwa ni krosi ya Mohamed Hussein 'Tshabalala'.

Dakika ya 13 mchezaji wa Majimaji, Samir Ruhava alikosa bao baada ya kupiga shuti kali lililotoka nje ya goli, ambapo Mwamuzi wa mchezo huo Alex Mhagi kutoka Mwanza alimpa kadi ya njano Frank Sekule wa Majimaji kwa kumchezea rafu Awadh Juma wa Simba.

Ajibu alikosa bao dakika ya 17 baada ya kupiga krosi aliyokuwa analenga kumpa Hamisi Kiiza ambapo mpira ulimpitiliza huku Kiiza tena akikosa bao dakika ya 24 baada ya kupiga shuti lililookolewa na kipa wa Majimaji, David Burhan.

Kiiza aliiandikia Simba bao la tatu ikiwa ni dakika ya 37 akipokea pasi ya Tshabalala wakati Burhan akiwa amesimama pembeni kidogo ya goli akijua kwamba Kiiza hataweza kupiga mpira na kufunga bao hilo.

Dakika ya 42, Ajibu alifunga bao la nne akipokea krosi iliyopigwa na Mwinyi Kazimoto ambaye aliipiga kwa kichwa na kuifanya Simba kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 4-0.

Katika kikosi cha leo cha Simba, Kerr aliamua kuwapumzisha baadhiya nyota wake Hassan Kessy, Said Ndemla, Juuko Murshid na kuwapa nafasi Emery Nimubona na Ajibu.

Simba ilipata bao la tano dakika ya 79 lililofungwa na Tshabalala baada ya mabeki wa Majimaji wakidhani kuwa ameotea huku Kiiza akifunga bao la sita dakika ya 80 ambapo Emery alipiga krosi iliyomkuta Kimwaga ambaye alishindwa kufunga baada ya kuzongwa na wachezaji wa Majimaji hivyo mpira ukampata Kiiza na kufunga.

Majimaji walipata bao la kufutia machozi dakika ya 88 kupitia kwa mchezaji wao Ditram Nchimbi baada ya kupiga mpira ambao kipa wa Simba, Vicent Angban aliutema.

Kipindi cha Kerr alifanya mabadiliko ambapo aliwatoa Jonas Mkude, Ajibu na Peter Mwalyanzi nafasi zao zilichukuliwa na Joseph Kimwaga,  Pape N'Daw na Simon Sserunkuma wakati kocha wa Majimaji, Mika Llonnstom naye akimtoa Idd Kipagwile na kuingia Marcel Bonaventure.


Post a Comment

 
Top