BOIPLUS SPORTS BLOG

By Sheila Ally, Dar Es Salaam

KIUNGO wa Yanga, Haruna Niyonzima jana alifunga ndoa na mkewe Uwineza Naillah na huenda akakosa mechi yao ya kesho dhidi ya Azam Fc huku ikielezwa kuwa kiungo huyo huenda akatua leo jijini Dar es Salaam.

Yanga itacheza kesho na Azam katika mwendelezo wa mechi za Ligi Kuu Bara ikiwa ni mechi yao ya sita kwa timu zote ambazo zina pointi 15 kila moja huku Yanga ikishika usukani kwani ina mabao mengi ya kufunga.

Awali ilielezwa kwamba Niyonzima alikuwa akipigiwa simu na uongozi wake bila kupatikana hewani na baadaye ilitolewa taarifa kwamba kulikuwa na matatizo ya usafiri wa kurudi nchini.

Imeelezwa kuwa kiungo huyo huenda akaingia usiku wa leo na tayari Kocha Mkuu wa Yanga, Hans Pluijm amemtoa kwenye mipango yake ya kesho.

Habari zaidi kutoka ndani ya Yanga zinasema kuwa Niyonzima aliaga kuwa anakwenda kuisadia timu yake ya Taifa ya Rwanda na hakuna aliyekuwa anafahamu kuwa anakwenda pia kufunga ndoa hiyo jambo ambalo limeonekana kuwakera viongozi wake kwani atakosa mechi muhimu na yenye upinzani mkubwa kwao.


Post a Comment

 
Top