BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda
STRAIKA wa zamani wa Simba na Yanga, Emmanuel Okwi jana aliwathibitishia mabosi wake wapya Sonderjyske ya nchini Denmark kuwa yeye ni moto wa kuotea mbali baada ya kuifungia timu hiyo mabao mawili katika ushindi wa mabao 6-2 dhidi Greve IF.

Katika mechi hiyo ya Kombe la Ligi iitwayo Landspokal, Sonderjyske ndio waliokuwa wa kwanza kuliona lango la Greve ambapo dakika ya 14 tu mshambuliaji Dalgaard aliipatia timu yake bao la kwanza kabla hajaongeza la pili dakika nne baadaye hivyo kuipeleka timu yake kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao hayo mawili.


Kipindi cha pili kilianza kwa Okwi kuweka wavuni bao la tatu na la kwanza kwake ikiwa ni dakika ya 61. Lakini wakati Sonderjyske wakiwa hawajamaliza furaha ya bao hilo, Larsson wa Greve aliipatia timu yake bao la kwanza ikiwa ni dakika moja tu baada ya Okwi kufunga.

Katika kuonyesha kuwa amepania kuivusha timu yake hadi hatua ya robo fainali ya ligi hiyo, Okwi iliipatia timu yake bao la nne katika dakika 64 kabla Simonsen na Hedegaard hawajaongeza mabao katika dakika za 68 na 83.

Greve walipata bao lao la pili na la mwisho dakika ya 90 na hivyo mechi hiyo kumalizika kwa Sonderjyske kuibuka na ushindi huo mnono.


Sonderjyske inayoshika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Denmark ijulikanayo kama Superliga, ilimnunua Okwi kutoka Simba kwa dau la dola 100000 sawa na  Sh. 220 milioni.

Post a Comment

 
Top