BOIPLUS SPORTS BLOG

NYOTA wa kutumainiwa wa TP Mazembe, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu leo wameonyesha kwanini wanacheza nje ya Tanzania kwa kuisaidia Stars kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi timu ya taifa ya Malawi 'The Flames' kwenye mchezo wa kufuzu kombe la dunia 2018. Mechi hiyo imechezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mfungaji wa bao la kwanza Mbwana Samatta akihojiwa na waandishi wa habari baada ya mchezo huo

Samatta ndiye alikuwa wa kwanza kuwainua mashabiki wa Stars kwa kuipatia bao safi dakika ya 18 ya mchezo akimalizia krosi ya Ulimwengu aliyekuwa mwiba kwa walinzi wa Flames.

Baada ya bao hilo Stars iliendelea kulisakama lango la vijana hao wa Malawi na dakika nne tu baada ya bao hili, shuti kali la mlinzi wa kushoto wa Stars Haji Mwinyi lililogonga mwamba na kurudi uwanjani lilimaliziwa kiufundi na Ulimwengu na kufanya Stars iende mapumziko ikiwa mbele kwa mabao hayo mawili.

Katika mchezo huo Kocha Mkuu wa Stars, Boniface Mkwasa aliwatumia viungo wawili tu wa kati hivyo kuwapa mwanya viungo wa Flame kumiliki eneo hilo kwa kipindi kirefu na kutengeneza mashambulizi mengi yaliyozaa kona tisa ambazo hazikuzaa matunda huku Stars ikipata kona tano tu.

Stars itaifuata Flames kwa mchezo wa marudiano wakiwa na mabao mawili mkononi hivyo kuhitaji sare ya aina yoyote au kufunga bao moja pekee ili wafuzu hatua inayofuata.

Katika mchezo huo Mkwasa aliwapumzisha Ulimwengu, Mrisho Ngassa na Farid Mussa huku nafasi zao zikichukuliwa na Ibrahim Ajibu, Salum Telela na Simon Msuva.

Post a Comment

 
Top