BOIPLUS SPORTS BLOG

SIMBA inatarajia kuondoka keshokutwa Jumapili kwenda jijini Mbeya kwa ajili ya kuzoea hali ya hewa ya huko kabla hawajawavaa Mbeya City na Prisons ambapo inasemekana kuwa kambi hiyo huenda ikawekwa  Tukuyu wilayani Rungwe.
Kesho asubuhi Simba wataendelea na mazoezi yao katika Uwanja wa Boko Veteran ambapo Jumapili wataanza safari hiyo ya kwenda kusaka pointi sita jijini humo.


Hii inaonyesha wazi kwamba Simba awamu hii wamepania pia kuondoa gundu katika mechi za mkoani ambapo Mbeya City imekuwa ikiwasumbua tangu ilipopanda daraja kushiriki Ligi Kuu Bara.
Simba haijawahi kuifunga mechi yoyote Mbeya City kwa misimu yao miwili iliyoshiriki ligi hiyo ambapo Simba hata uwanja wao wa nyumbani wa Taifa imekuwa ikipoteza mechi zake kwa Mbeya City ambayo ipo chini ya kocha Juma Mwambusi anayetajwa kutua Yanga muda wowote kwani mazungumzo yao yamefikia pazuri.
Habari kutoka ndani ya Simba zimesema kuwa baada ya majadiliano kati ya Kocha Mkuu Dylan Kerr na viongozi wake wamekibaliana kwa pamoja kuwa timu hiyo iondoke Jumapili.


Mechi yao na Mbeya City itachezwa Oktoba 17 wakati mechi na Prisons itachezwa Oktoba 21, mechi zote zitachezwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Mchakato wa kuweka kambi mjini Tukuyu ulianza tangu wiki iliyopita lakini viongozi walikuwa wakimsubiri Kerr ili kupitisha mapendekezo hayo ambapo leo jioni walikutana na kuamua kwa pamoja.
''Timu kesho itafanya mazoezi yake asubuhi pale Boko kama kawaida ila safari ya kwenda Mbeya itakuwa ni Jumapili kama hakutakiwa na mabadiliko yoyote, tunawahi kwenda huko ili kuzoea hali ya hewa na mazingira,'' kilisema chanzo hicho.

Post a Comment

 
Top