BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally, Dar.

KOCHA Mkuu wa Simba, Dylan Kerr huenda akafungishiwa virago vyake muda wowote kuanzia sasa kwa kile kilichoelezwa kuwa kikosi chao kimeanza kufanya vibaya kutokana na kutopata mazoezi ya nguvu na kocha huyo amekuwa mbishi kuongeza dozi.

Mbali na sababu hiyo imeelezwa kuwa kwasasa wachezaji wa Simba hawana nidhamu jambo ambalo kocha huyo amekuwa akilitazama bila kulichukulia hatua huku wengine wakitoroka kwenda kwenye kumbi za starehe pasipo kuonywa vikali.

Habari kutoka ndani ya Simba zinasema kuwa awali kocha huyo alipewa mechi mbili ambazo ni za jijini Mbeya, ile ya Mbeya City na ya Prisons lakini sasa wamempa muda mpaka ligi itakaposimama na yeye ndipo aondoke moja kwa moja.

"Wachezaji wanakosa pumzi kabisa kipindi cha pili, mazoezi anayowapa ni mepesi mno na ni mbishi kupokea mawazo, ni lazima timu iwe na kocha wa viungo ili kurejesha pumzi kwa wachezaji, lakini pia amewaacha wachezaji wafanye vile wanavyotaka pasipo yeye kuwa mkali.

"Alipewa mechi mbili za Mbeya lakini tumeona ni vyema amalizie zilizobaki kwani tunakwenda mapumzikoni muda si mrefu, hivyo hatarudi tena inabidi kujipanga kupata kocha mwingine pamoja na wa viungo, kuna kikao kinaweza kufanyika hapo baadaye ambacho kitatoa picha halisi ya nini kitafanyika wakati wa mapumziko," alisema kiongozi huyo.

Kerr mwenyewe amesema anafahamu kinachoendelea kwake kuwa huenda ataondoka muda wowote, hivyo anajiandaa kwa lolote.

Simba imecheza mechi saba ambapo imepoteza mechi mbili na kushinda mechi tano zilizowafanya wakusanye pointi 15 na kushika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara wakitanguliwa na Yanga, Azam ambao wana pointi 19 huku Stand United ikishika nafasi ya tatu kwa pointi 15.

Mechi ambazo Kerr atazisimamia kabla ya ligi kusimama ni dhidi ya Coastal Union na Majimaji kwani mechi yao na Azam imesogezwa mbele.

Post a Comment

 
Top