BOIPLUS SPORTS BLOG

By Karim Boimanda, Dar Es Salaam


Marehemu Emmanuel Makaidi

RAIS wa Klabu ya Simba na uongozi, wanachama na wapenzi wa klabu umetuma salamu za pole kwa familia ya Marehemu Emmanuel Makaidi aliyefariki leo mchana na kuupokea msiba huo kwa masikitiko makubwa ya kuondokewa na Mwenyekiti wao wa zamani wa klabu hiyo.Msiba huo umetokea leo mchana kwenye hospitali ya Nyangao mkoani Lindi


Mzee Makaidi licha ya kuwahi kuwa Mwenyekiti wa Simba pia ni mwanachama wa maisha wa klabu.
Msiba huu mzito umetokea katika kipindi hiki kigumu ambacho klabu bado ilikuwa inamhitaji sana kiongozi huyo mahiri kwenye medani za michezo na kisiasa.

Kihistoria Klabu ya Simba inamkumbuka jemedari huyo kwa msimamo thabiti hususan miaka ya sabini wakati yeye na viongozi wenzake Marehemu Alfred Sanga na Jimmy David Ngonya waliposimama imara wakati wa mgawanyiko kwenye klabu ambao hatimaye ulizaa klabu nyingine ubavuni mwa Simba iliyoundwa mwaka 1976 na kujulikana kwa jina la Nyota nyekundu.

Simba tutaendelea kumkumbuka Mzee Makaidi kwa ucheshi na utani wake sambamba na mipango yake ya kuifanya Simba kuwa klabu inayojitegemea.

Mwanachama huyo wa zamani wa tawi maarufu la klabu ya Simba liitwalo Shibamu pia hatasaulika kwa kutoa ushauri wake kwa viongozi wa sasa wa klabu ambayo aliishabikia katika maisha yake yote.

''Hakika bado Wanasimbazi walimhitaji mzee Makaidi ambaye sisi wajukuu zake tulipenda kumtania kwa jina la Motomoto ila mungu alimhitaji zaidi. Kwa niaba ya uongozi mzima wa Simba tunatoa pole kwa wafiwa hususan mkewe (Mama Modesta) na watoto pamoja na familia yote ya marehemu,'' alisema Aveva.

Uongozi wa Simba upo pamoja na wafiwa kwenye kipindi hiki kigumu na utashiriki kwa hali na mali kwenye msiba huu mzito kwa wapenda soka wote nchini.

Post a Comment

 
Top