BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally, Mbeya.


Mohamed Hussein 'Tshabalala'  akipambana na Haruna Moshi 'Boban'  wa City

SIMBA leo imevunja mwiko katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya baada ya kuifunga Mbeya City bao 1-0 ikiwa ni mwendelezo wa mechi za Ligi Kuu Bara.

Tangu Mbeya City ipande daraja haijawahi kufungwa na Simba ambapo mara nyingi Wekundu wa Msimbazi wamekuwa wakipata matokeo ya sare ama kufungwa.

Matokeo hayo yameifanya Simba iendelee kushika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 15 wakati Yanga wanaendelea kukaa kileleni ikiwa na pointi 16 sawa na Azam ambao wanashika nafasi ya pili.

Simba ndiyo iliyokuwa ya kwanza kulifikia lango la City ambapo katika dakika ya pili tu ya mchezo ilipata kona iliyopigwa na Mohamed Hussein 'Tshabalala' na kumkuta Juuko Murshid aliyeukwamisha wavuni.

Baada ya bao hilo City wakiongozwa na kiungo wa zamani wa Simba Haruna Moshi 'Boban' walilianza kuliandama lango la Simba na kufanya mashambulizi kadhaa yaliyozaa kona kadhaa ambazo hazikuzaa matunda.

Simba licha ya kuchezesha viungo watano ukimuacha Mwinyi Kazimoto ambaye pia alichezeshwa kama mshambuliaji wa pili nyuma ya Mussa Hassan 'Mgosi', bado ilipata wakati mgumu mbele ya viungo watatu wa City ambao ni Boban, mkongwe Steven Mazanda na Christian Sembuli.

Mshambuliaji wa Simba Mussa Hassan 'Mgosi' akijaribu kumtoka mlinzi wa City

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kucheza mpira wa kasi huku Simba wao  wakifanya mashambulizi kadhaa ambayo yalionekana wazi kuwa yalitokana na mipango mibovu. 

Mabadiliko ya kumtoa Abdi Banda na nafasi yake kuchukuliwa na Peter Mwalyanzi yaliisaidia sana Simba na katika kipindi hicho walifanikiwa kulifikia lango la City mara kadhaa ingawa mshambuliaji wa kati Mgosi hakuweza kuipatia Simba bao.

Katika dakika za majeruhi Simba walirudi nyuma kulinda bao lao hivyo kuwafanya City kuhamishia kambi langoni mwa Simba ambapo katika dakika 89 nusura City wasawazishe baada ya kufanya shambulizi kali lililowafanya mashabiki wainuke vitini wakiamini timu yao inasawazisha.

Mabadiliko aliyoyafanya  Dylan Kerr ni kuwatoa Banda, Jonas Mkude na Mwinyi Kazimoto ambapo nafasi zao zilichukuliwa na Peter Mwalyanzi, Awadhi Juma na Joseph Kimwaga wakati kocha wa Mbeya City, Abdul Migange naye alifanya mabadiliko kwa kuwatoa Christian Sembuli, Haruna Moshi 'Boban' nafasi zao zilichukuliwa na Abdallah Seif na Hamad Kibopile.

Post a Comment

 
Top