BOIPLUS SPORTS BLOG

MENEJA wa Manchester United Louis van Gaal amejaribu kumlinda Wayne Rooney dhidi ya upinzani anaopata kutoka kwa mashabiki na waandishi baada ya mshambuliaji huyo kushindwa kuonyesha uwezo katika sare ya 0-0 dhidi ya Manchester City

United walimiliki mpira kwa kiwango kikubwa katika mechi hiyo kubwa ya 170 Jumapili katika uwanja wa Old Trafford, lakini walilazimika kusubiri hadi dakika za mwisho kujaribu kutengeneza nafasi, wakati Jesse Lingard akigonga besela na Chris Smalling akimlazimisha Joe Hart kuokoa hatari golini.Mchezo wa tatu mfululizo Rooney akianzishwa katika safu ya ushambuliaji, lakini akifichwa na kazi nzuri ya mchezaji mwenzake Anthony Martial, aliyekuwa akitokea kushoto, ambaye pia alikuwa mchezaji hatari zaidi  United baada ya kumchongea Lingard pasi hatari ambayo ilileta madhara kwa Hart.

Van Gaal alikataa kujadili ufanisi wa Rooney, hata hivyo, aliuambia mkutano wa waandishi baada ya mechi: “Kila wiki nahitajika kuzungumza kuhusu Rooney, kwa nini?”

Alipoambiwa kuwa ni kwa sababu nahodha huyo wa United ni moja ya wachezaji nyota wa timu hiyo, Van Gaal alimjibu aliyekuwa akimhoji: “Basi inakubidi uandike. Ni maoni yako.”
“Sikupi majibu zaidi kuhusu Wayne Rooney kwa sababu naugua kwa maswali hayo.”

Ikiwa ni siku moja baada ya kutimiza miaka 30, Rooney alikuwa akitarajia kudumisha rekodi yake ya kufunga magoli 11 katika mechi kubwa na kufikia idadi ya magoli ya Denis Law ya mabao 237 Man United, lakini hakufanikiwa kwani hakuweza hata kujaribu kupiga shuti langoni.

Lakini si yeye pekee aliyeshindwa kwani Manchester United walilenga goli mara moja tu, kupitia Smalling na Van Gaal alibainisha kuwa aliwauliza wachezaji wake muda wa mapumziko: “Kwa nini hampigi mashuti?”

Lakini malalamiko yake hayakuishia hapo, alieleza pia kutofurahishwa na uamuzi wa Mark Clattenburg kutowapa United penalti mapema kipindi cha pili baada ya Ander Herrera kufanyiwa madhambi na Raheem Sterling.

“Hatuna bahati hata hivyo kwa sababu niliona kwenye video kwamba Herrera alipata penalti, lakini mwamuzi hakutupa stahiki yetu,” alisema

United wameshindwa kujaribu kufunga goli kipindi cha kwanza kwenye mechi ya Ligi ya Uingereza tangu msimu wa 2003-04, kwani iliwachukua hadi dakika ya 82 kwa pande zote kufanikiwa kupiga mashuti yaliyolenga goli, baada ya Jesus Navas akitokea benchi kumjaribu David De Gea.


Meneja wa Man City, Manuel Pellegrini amesema hakuona kama Herrera alistahili penalti na amemsifu Clattenburg kwa kazi yake “nzuri”.

Timu yake imefunga magoli 11 katika mechi mbili za nyma, wakiisambaratisha Newcastle United 6-1 na kuiburuza Bournemouth 5-1, na Pellegrini alikiri kuwa hakufurahia mechi hiyo ya Jumapili.

Lakini amefurahia jinsi mabeki wake walivyowadhibiti Man Utd walipoongeza mashambulizi kipindi cha pili.

“Sijui kama kweli tumecheza katika kiwango chetu kizuri,” alisema Mchile huyo, ambaye timu yake imerudi kileleni msimamo wa ligi, juu ya Arsenal kwa tofauti ya magoli, na United wakibaki nafasi ya nne.

“Mara kwa mara nasoma sana vinachosema vyombo vya habari timu zinapopata pointi katika mechi za ugenini kuwa zimetumia mbinu nyingi na akili

“Silipendi jambo hili, si kawaida yetu kufanya hivi, lakini tunapohitaji kufanya hivyo, tunaweza. Pointi moja si mbaya. Tunaendelea kukaa kileleni.”

Post a Comment

 
Top