BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally, Mbeya.

USHIRIKINA. Leo katika mechi ya Simba na Prisons kumetokea na vituko mbalimbali hata kabla ya mechi hiyo kuanza, vituko ambavyo vilikuwa vinaashiria imani za kishirika. Lakini kubwa zaidi ni lile lililotokea kwa straika wa Simba, Pape N'daw ambaye imeelezwa kukamatwa na hirizi.

Ilikuwa hivi. Dakika ya 33 wakati Simba ikienda kupiga mpira wa kona ambao ulipigwa na Mohamed Hussein 'Tshabalala' lakini kabla ya kuupiga mpira huo, kiungo wa Prisons Jumanne Alfadhili alianza kuvutana jezi na N'daw ili kumzuia asilete madhara langoni kwao ndipo ishu ya hiziri ilianzia hapo.

Ilielezwa kuwa wachezaji wa Prisons walimlalamikia mwamuzi kuwa N'daw alikuwa amevaa hirizi ambapo mwamuzi alilazimika kumtoa nje ya uwanja na kumpeleka chumba cha kubadilishia nguo na kumkagua ndipo ilipobainika kuwa N'daw alikuwa na kitu kilichosadikika kuwa ni hirizi na alikifunga kiunoni.

Mwamuzi alilazimika pia kumwita kamisaa wa mchezo huo ili ashuhudie na ndipo aliamuriwa avue ili akaendelee na mchezo huku akipewa kadi ya njano kwa kuvaa kitu hicho kinyume na sheria za mchezo.

BOIPLUS ilimfuata mmoja wa wasimamizi wa mchezo huo ambaye hakutaka jina lake litajwe kutokana na sheria zao za kazi, alikiri kwamba "Ni kweli amekutwa na kitu ambacho siwezi kusema moja kwa moja kama hirizi au lah na hizo ni imani zao za kishirikina, nampongeza mwamuzi amefanya busara kumtoa uwanjani kuja kumkagulia huku ndani maana ingekuwa ni aibu kubwa na udhalilishaji kumvua nguo mbele za watu.

"Kisheria hairuhusiwi kwa mchezaji yoyote kuingia na kitu kinachoonekana mwilini mwake maana inaweza kuwa hatari kwa wenzake, hivyo hilo ni kosa kikanuni," alisema.

Hata hivyo BOIPLUS ilifanya uchunguzi juu ya hilo na kugundua kuwa kitu alichokuwa amevaa Pape huwa anavaa siku zote anapokuwa mazoezini na hata kwenye mechi ikiwa kama kinga yake ya mwili kama alivyoeleza.

Post a Comment

 
Top