BOIPLUS SPORTS BLOG

LIGI Kuu ya Vodacom (VPL) inatarajiwa kuendelea kesho Jumatano kwa michezo minne kuchezwa katika viwanja tofauti nchini, huku timu nane zikisaka kupata pointi tatu muhimu.


Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Yanga  watawakaribisha Toto Africans, mchezo utakaonza saa 10:30 jioni, mjini Shinyanga Stand United watakuwa wenyeji wa Majimaji katika Uwanja wa Kambarage mjini humo.

Tanzania Prisons watawakaribisha Simba SC katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, huku Wagosi wa Kaya, Coastal Union wakiwakaribisha Kagera Sugar katika uwanja wa Mkwakani jijini Tanga.

Alhamis ligi hiyo itaendelea kwa michezo minne pia kucheza katika viwanja mbalimbali, JKT Ruvu wataikaribisha Mtibwa Sugar uwanaj wa Karume jijini Dar es salaam, Mwadui FC watacheza dhidi ya Mgambo Shooting katika uwanja wa Mwadui Complex mjini Shinyanga.

Jijini Mbeya, Mbeya City watawakaribisha African Sports katika uwanja wa Sokoine, huku Ndanda FC wakiwa wenyeji wa Azam FC katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

Wakati huo huo, mechi za raundi ya 11 za Ligi Kuu ya Vodacom zilizokuwa zichezwe Novemba 7 na 8 sasa zitafanyika Desemba 12 na 13 kupisha maandalizi ya Taifa Stars ya mechi za mchujo za Kombe la Dunia.

Taifa Stars inatarajia kuingia kambini mapema mwezi ujao kujiandaa na mechi ya kwanza dhidi ya Algeria ambayo itafanyika Novemba 14 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Timu hizo zitarudiana nchini Algeria, Novemba 17 mwaka huu.

Mechi hizo za Vodacom zitakazochezwa Desemba 12 ni kati ya Mgambo Shooting na Yanga (Tanga), Kagera Sugar na Ndanda (Tabora), Stand United na Mwadui (Shinyanga), Mbeya City na Mtibwa Sugar (Mbeya), Azam na Simba (Dar es Salaam) na Majimaji na Toto Africans (Songea). Mechi za Desemba 13 ni kati ya JKT Ruvu na Tanzania Prisons (Dar es Salaam), na Coastal Union na African Sports (Tanga).

Pia mechi tatu za raundi ya sita ambazo hazikuchezwa Oktoba 4 kupisha mechi ya Taifa Stars na Malawi sasa zitafanyika Desemba 16. Mechi hizo ni kati ya Azam na Mtibwa Sugar (Dar es Salaam), na African Sports na Yanga (Tanga), mchezo kati ya Ndanda na Simba (Mtwara utapangiwa tarehe ya kuchezwa.

Nayo mechi namba 59 kati ya JKT Ruvu na Mtibwa Sugar iliyokuwa ichezwe Oktoba 21 Uwanja wa Karume, Dar es Salaam imesogezwa mbele kwa siku moja hadi Oktoba 22 mwaka huu ili kuipa nafasi ya mapumziko JKT Ruvu ambayo jana ilicheza mechi yake ya raundi saba mkoani Shinyanga

Post a Comment

 
Top