BOIPLUS SPORTS BLOG

KIUNGO wa Azam FC, Salum Abubakar 'Sure Boy' amesema kuwa hawataki kuchafua rekodi yao ya kufungwa kwenye mechi za Ligi Kuu Bara na kutamka kwamba Yanga wanaiogopa Azam ndiyo maana wanaizungumzia sana.

Sure Boy amesema kwamba mechi hiyo ambayo itachezwa keshokutwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam itakuwa ngumu kwa pande zote mbili kwani hakuna atakayekubali kufungwa kirahisi ambapo timu hizo zimecheza mechi tano kila moja huku zote zikiwa na pointi 15. Yanga ipo kileleni kwasababu ina mabao mengi ya kufunga wakati Azam inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Alisema kuwa kitu pekee kitakachowabeba kushinda mechi hiyo ni kutokana na maandalizi mazuri waliyoyafanya na wapo vizuri kila idara japokuwa hawaibezi Yanga kwani hata wao wapo vizuri.

"Mechi itakuwa ngumu sana kwasababu wote tumefanya maandalizi ya kutosha, sisi hatujapoteza na hata Yanga hawajapoteza hivyo kila mmoja hawezi kukubali kuchafua rekodi yake, tuliwafunga kwenye Kombe la Kagame na wao walitufunga kwenye Ngao ya Hisani hapo tu inaonyesha ni jinsi gani kila mmoja ana upinzani kwa mwenzake.

"Tunawaheshimu Yanga kwasababu ni timu kubwa ila hata wao wanatuogopa pia ndiyo maana wanatuzungumzia sana, hiyo inaonyesha ni kiasi gani tupo vizuri, mashabiki wetu watarajie ushindi na waje kwa wingi kutusapoti, ushindi upo na utapatikana, timu yetu imekamilika kila idara," alisema Sure Boys.

Azam wanaendelea na mazoezi yao katika Uwanja wao wa Chamazi wakati Yanga wao ambao tayari wameimarisha Benchi la Ufundi kwa kumwajiri Juma Mwambusi aliyechukuwa nafasi ya Boniface Mkwassa ambaye sasa ni Kocha wa Taifa Stars, wanafanya mazoezi yao Uwanja wa Boko Veterani.

Post a Comment

 
Top