BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda, Dar.

YANGA noma. Leo bila huruma imeifanyia mauaji Toto Africans ya jijini Mwanza kwa kuitandika mabao 4-1. Mchezo huo wa ligi kuu ya Vodacom ulipigwa katika dimba la Taifa jijini Dar Es Salaam.

Kipindi cha kwanza kilianza kwa kasi kwa timu kushambuliana kwa zamu lakini Yanga ndio waliofanikiwa kupata bao la mapema lililowekwa nyavuni na mlinzi Juma Abdul katika dakika ya tisa akiunganisha kwa shuti kali mpira wa kona uliochongwa na Haruna Niyonzima.

Baada ya bao hilo Yanga waliendelea kuliandama lango la Toto ingawa utulivu wa walinzi wake ulizima mashambulizi mengi. Toto iliyo na wachezaji sita waliopita Simba ilionyesha kandanda safi la pasi za chini chini na kulifikia lango la Yanga mara kadhaa ingawa walishindwa kupata bao kwa sababu zilizoonekana wazi kuwa ni kukosa uzoefu kwa wachezaji wao wengi.

Wakati dakika 45 zikiwa zinaenda ukingoni, Yanga walipata penati kufuatia straika Donald Ngoma kuangushwa kwenye eneo la hatari la Toto. Mlinda mlango wa Toto aliibuka shujaa kwa kuokoa penati hiyo iliyopigwa na Ngoma mwenyewe.

Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kulishambulia lango la Toto ambapo katika dakika ya 48 Simon Msuva aliambaa na mpira upande wa kulia na kupiga shuti ambalo kipa wa Toto alipishananalo na kuiandikia Yanga bao la pili

Katika dakika ya 52 aliipatia Toto bao la kufuatia machozi akimalizia mpira uliotemwa na Ally Mustafa 'Barthez'.

Mabao mengine ya Yanga yalifungwa na mshambuliaji hatari Amiss Tambwe katika dakika 81 kwa kichwa na Msuva aliyemalizia karamu hiyo katika dakika ya  90 akimalizia kiustadi krosi ya Mbrazil Andrey Coutinho.

Mwamuzi wa mchezo huo alimzawadia mlinzi wa Toto Miraji Adam kadi ya pili ya njano kisha nyekundu katika dakika za lala salama.

Post a Comment

 
Top