BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally
JKT Ruvu imempa mkataba wa miezi sita mchezaji wa Accacia Stand United, Hassan Dilunga lakini viongozi wa timu hiyo ya Shinyanga wametamka kwamba Maafande hao imekula kwao kwani mchezaji huyo wana mkataba naye ambao alisaini Agosti mwaka huu akitokea Yanga.

Mratibu wa Accacia Stand United, Mbasha Matutu alisema kuwa Dilunga alisaini mkataba wa mwaka mmoja kwao hivyo amewadanganya viongozi wa JKT Ruvu na kama amewapelekea barua ya kuonyesha kuwa yupo huru basi barua hiyo ni feki.

Mbasha alisema kuwa kama JKT Ruvu hawatakwenda kufanya mazungumzo na Stand basi itakula kwao kwani ikifika wakati wa kuweka pingamizi mchezaji huyo atawekewa pingamizi na leseni yake ya kumruhusu kucheza haitatolewa.

Hassan Dilunga


''Waache wamsajili ila itawapa shida hapo baadaye. Maana sisi tutahitaji fedha yoyote kama watakuja kumalizia mazungumzo ya kumsajili wakati tayari wamempa mkataba huko, Dilunga ana mkataba na sisi hivyo tunasubiri muda wa pingamizi ufike.

''Jambo ambalo linaweza kutokea ni hasara kwa mchezaji na klabu iliyomsajili maana hataweza kucheza sisi tuna leseni yake na hakuna kiongozi aliyetoa barua ya kuonyesha kuwa yupo huru na kama kuna barua wamepewa hiyo ni feki, na utaratibu ni lazima tumuondoe kwanza kwenye mfumo wetu wa usajili unaotambulika na TFF ndipo aweze kucheza timu nyingine,'' alisema Mbasha.

Tangu Stand United wamecheza mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba na kufungwa bao 1-0, Dilunga alijiondoa kwenye kikosi hicho baada ya kutofautiana na kocha wao Patrick Leiwig walipodai mabaki ya fedha zao za usajili pamoja na Hamad Ndikumana hakujiunga na timu hiyo mpaka sasa.

Tayari uongozi wa Stand United umeachana na beki wao Ndikumana na umedai kuwa Dilunga alimaliziwa fedha yake ya usajili pamoja na kulipwa mishahara yake ya miezi miwili aliyokuwa akidai ambayo walimsitishia kama adhabu ya kuondoka kambini.

Post a Comment

 
Top