BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally
MABINGWA wa Kombe la Kagame, Azam FC wamepanda kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom baada ya kuifunga Toto Africans ya Mwanza mabao 5-0, mechi hiyo imechezwa Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam na kuifanya Azam ipande kileleni ikiwa na pointi 25 huku Yanga wakishuka nafasi ya pili wakiwa na pointi 23.


Somari Kapombe ndiye aliyeanza kutikisa nyavu za wapinzani wao dakika ya 32 kwa kichwa akipokea krosi ya Farid Musa wakati bao la pili Kapombe alilifunga dakika ya 34 akipokea pasi nzuri ya kichwa ya Didier Kavumbagu.

Dakika ya 45, Kipre Tchetche aliifungia Azam bao la tatu akipokea pasi ya Kavumbagu na kwenda mapumziko ikiwa inaongoza kwa mabao 3-0 lakini mara baada ya kurudi kipindi cha pili dakika ya 47, beki wa Toto, Erick Mlelo alijifunga baada ya Ramadhan Singano wa Azam kupiga krosi iliyompata Mlelo na kujifunga.

Kavumbagu aliiandikia Azam bado la tano dakika ya 62 ambalo lilitokana na piga nikupige langoni mwa Toto Africans ingawa Aishi Manula na Jean Mugiraneza 'Migi' waliumwa tumbo ghafla na hivyo kulazimika mchezo huo kusimama kwa dakika tano kwani tayari Azam walikuwa wamemaliza wachezaji wote wa akiba.

Prisons wao wameshindwa kutamba mbele ya Ndanda FC katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya kulazimisha sare ya bao 2-2, bao la kwanza la Prisons lilifungwa dakika 17 mfungaji akiwa ni Lambat Sabianka aliyefungwa kwa kichwa akiunganisha krosi ya iliyopigwa na Mohammed Mkopi wakati bao la pili lilifungwa na Jeremiah Juma dakika ya 23 aliyempiga kanzu kipa wa Ndanda, Jackson Chove.

Kipindi cha pili, beki wa Prisons James Mwasote alikuwa akijaribu kuokoa mpira uliotemwa na kipa wao Aron Kalambo ndipo kipa huyo katika harakati za kuudaka aliukosa ukarudi ndani na kumpata Mwasote ambaye alijikuta akijifunga dakika ya 52.

Dakika ya 68, Ndanda walisawazisha bao la pili mfungaji akiwa ni Burhan Rashid aliyepiga mpira wa kumalizia baada ya kipa  wa Prisons kuutema mpira wa shuti kali lililopigwa na Omega Seme ambayo ilikuwa ni faulo aliyopigwa nje kidogo ya 18, Prisons walikosa penalti dakika ya 80 iliyopigwa na Mkopi.

Post a Comment

 
Top