BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda
VIGOGO wa soka barani Ulaya, FC Barcelona leo wamewaangushia kipigo kikali cha mabao 4-0 mahasimu wao Real Madrid katika mchezo wa ligi kuu ya Hispania, La Liga. Mchezo huo ulichezwa katika dimba la nyumbani la Madrid, Santiago Bernabeu.

Barcelona waliotawala mchezo huo kwa kiasi kikubwa walitingisha nyavu za Madrid katika dakika ya 10 tu kupitia kwa Luiz Suarez aliyeitumia vema pasi ya Sergi Robert.Barcelona waliendelea kuliandama lango la Madrid huku wakitawala eneo la kiungo na kulifikia lango la Madrid kila mara.  

Kocha wa Barca Luis Enrique aliamua kumpumzisha Javier Mascherano ambaye alipata majeraha baada ya kugongana na James Rodrigues huku nafasi yake ikichukuliwa na Heremy Matheu. 


Neymar Junior aliwainua mashabiki wachache wa Barca waliokuwepo uwanjani hapo kwa bao safi katika dakika ya 38 akimalizia pasi nzuri ya Iniesta huku walinzi wa Madrid wakiamini alikuwa ameotea. Hii ilikuwa ni mara baada ya Benzema kukosa bao la wazi kuufuatia shambulizi kali langoni mwa Barca.

Dakika ya mwisho ya kipindi cha kwanza Marcelo alifanya kazi ya ziada kwa kuokoa bao la wazi baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa Madrid.


Kipindi cha pili Barcelona waliendelea kumiliki mpira katika eneo la kiungo hivyo kuwafanya wafanikiwe katika kila walichopanga huku wakitibua kila mpango wa Madrid.

Hali hii ilipelekea Barcelona waendelee kupata mabao mengine mawili kupitia kwa Andres Iniesta na Suarez.

Katika mchezo huo refa aliwaonyesha kadi za njano James, Sergio Ramos na Daniel Carvajal wa Madrid na kwa upande wa Barvelona ni Alves na Sergio Busquets huku Isco akizawadiwa kadi nyekundu.

Post a Comment

 
Top