BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally
BEKI wa African Sports ya jijini Tanga, Novat Lufungo ametua Simba kwa dau la Sh 10 milioni na tayari jioni ya leo amejiunga na kikosi hicho kilichopiga kambi yake visiwani Zanzibar.

Simba ilianza kumuwinda beki huyo kabla hata ya dirisha dogo la usajili kufunguliwa ambapo leo hii wamemaliza kazi hiyo na kumsafirisha kwenda Zanzibar.

Chanzo cha habari kutoka Simba kilisema kuwa mchezaji huyo amepewa  mkataba wa miaka miwili ambao ataanza kuutumikia Ligi Kuu Bara itakapoanza Desemba 12 huku timu hiyo ikianza na Azam FC.

''Tayari amejiunga na timu huko Zanzibar jioni ya leo, kila kitu kipo vizuri kwa upande wa usajili wake na tumemalizana na klabu yake hivyo ni mchezaji wetu halali,'' alisema kigogo huyo.

BOIPLUS ilimtafuta kiongozi wa African Sports Abdul Bosnia ambaye ni Makamu Mwenyekiti alikiri kumwachia mchezaji huyo akacheze Simba.

''Ni kweli amejiunga Simba na sisi tumemalizana na viongozi wa Simba. Kuhusu mkataba aliopewa hayo tumemwachia mchezaji mwenyewe amalizane nao, tumempa uhuru wa yeye kufanya uamuzi wake japokuwa kuna mambo huwa tunamuongoza, sisi tulimsajili kwa mkataba wa mwaka mmoja,'' alisema Bosnia.

Kwa upande wa Nova yeye alisema kuwa ''Kweli nipo kambini ila bado sijasaini mkataba lakini naamini mambo yatakuwa mazuri,''.

BOIPLUS ina uhakika kuwa Nova amesaini mkataba huo na Simba leo kabla ya kwenda kujiunga na kambi hiyo japokuwa mchezaji huyo amefanya siri.

Post a Comment

 
Top