BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda, Lubumbashi
MMILIKI wa Klabu ya TP Mazembe ya hapa Lubumbashi DR Congo, Moise Katumbi amefunguka na kusema hakuna anayewafikia washambuliaji wake Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu kwa nidhamu ndani ya timu hiyo.

Akizungumza na BOIPLUS wakati wa mazoezi ya leo jioni yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Mazembe unaomilikiwa na klabu hiyo, Katumbi alisema nidhamu ya wachezaji hao wa kitanzania ni ya juu na anaamini hiyo ndiyo inayowafanya wazidi kung'ara.


"Ukizungumzia kiwango cha Samatta na Ulimwengu basi unazungumzia nidhamu yao, sijawahi kusikia tatizo lolote kwa vijana hawa. Wamekuwa kama watoto wangu wa kuwazaa, kama wachezaji wote wa Afrika wangekuwa na nidhamu ya vijana hawa wa Tanzania basi soka la Afrika lingefika mbali,'' alisema Katumbi

Mazembe inajiandaa na mechi ya marudiano ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya USM Alger ya Aljeria, itaingia dimbani Jumapili keshokutwa ikiwategemea zaidi Samata na Ulimwengu katika safu ya ushambuliaji.

Akizungumzia suala la Samatta kuondoka Mazembe, Katumbi alikiri kuwa ameshapokea ofa kutoka timu nyingi za Ulaya na muda si mrefu atamruhusu straika huyo kuondoka kwa roho nyeupe.


''Amefanya kazi kubwa Mazembe, ameipatia mafanikio mengi, acha sasa aende akafaidi maisha mengine Ulaya. Sina tatizo na yeye kuondoka, ila kama mzazi siwezi kumuacha aende popote, ni lazima nihakikishe anaenda sehemu ambapo ataitangaza Tanzania na Mazembe,'' alisema Katumbi

Timu hiyo itafanya mazoezi ya mwisho kesho asubuhi kabla ya kuwapisha USMA nao wafanye mazoezi jioni katika Uwanja huo unaomilikiwa na matajiri hao wa Jiji la Lubumbashi.

BOIPLUS itakuletea kila kinachojiri kuanzia kwenye maandalizi hadi kumalizika kwa mechi hiyo ya fainali

Post a Comment

 
Top