BOIPLUS SPORTS BLOG

KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’, Abdallah Kibadeni ametangaza kikosi cha wachezaji 21 kujiandaa na michuano ya Kombe la Chalenji itakayoanza kutimua vumbi Jumamosi Novemba 21, nchini Ethiopia.

Kibadeni anayesaidiwa na kocha msaidizi Juma Mgunda, amesema wachezaji aliowaita wapo katika hali nzuri na wamekuwa wakifanya mazoezi na kikosi cha Taifa Stars ambapo wao kama benchi la ufundi wamepata nafasi ya kuwa nao kwa muda mrefu na kutambua maendeleo yao.


“Tumechagua wachezaji kulingana na mahitaji ya timu, tumekua na wachezaji hawa kwa muda mrefu katika vipindi mbalimbali, tuna amini tuliowachagua watafanya vizuri katika michuano hiyo mikongwe barani Afrika” amesema Kibadeni.

Wachezaji walioitwa ni magolikipa, Ally Mustafa (Yanga) na Aishi Manula (Azam), Said Mohamed (Mtibwa Sugar), walinzi Shomari Kapombe (Azam), Hassan Kessy (Simba), Mohamed Hussein (Simba), Hassan Isihaka (Simba), Salim Mbonde (Mtibwa), Juma Abdul (Yanga) na Kelvin Yondani (Yanga).

Viungo Himid Mao (Azam), Jonas Mkude (Simba), Said Ndemla (Simba), Salum Telela (Yanga), Salum Abubakar (Azam), Deus Kaseke (Yanga), washambuliaji John Bocco (Azam), Elias Maguri (Stand United), Ibrahim Hajibu (Simba), Malimi Busungu (Yanga) na Saimon Msuva (Yanga), ambapo Kilimanjaro Stars imepangwa kundi A, lenye wenyeji Ethiopia, Rwanda na Somalia.

Wachezaji Said Mohamed, Juma Abdul, Hassan Kessy, Hassan Isihaka, Salum Abubakar na Ibrahim wanaendelea na mazoezi jijini Dar es Salaam chini ya kocha msaidizi Mgunda wakati wanawasubiri wachezaji wengine walioko nchini Algeria na kikosi cha Taifa Stars.

Kundi B lina Bingwa Mtetezi Kenya, Burundi, Uganda na Zanzibar, huku kundi C likiundwa na timu za Sudan, Sudani Kusini, Djibouti na waalikwa wa michuano hiyo timu ya taifa kutoka Malawi.

Post a Comment

 
Top