BOIPLUS SPORTS BLOG

STRAIKA wa Simba', Hamis Kiiza 'Diego' jana ameendelea kuonyesha umuhimu wake ndani ya Simba baada ya kuifungia timu hiyo mabao mawili kati ya sita kwenye mechi yao dhidi ya Majimaji ya Songea. Mabao mengine yalifungwa na Ibrahim Ajibu aliyefuga mabao matatu huku Mohamed Hussein 'Tshabalala akifunga moja.

Akizungumza na BOIPLUS mara baada ya mchezo huo kumalizika, Kiiza ambaye jana alikabidhiwa zawadi yake ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Vodacom mwezi Septemba, alisema anafurahi kuona anaisaidia timu yake kupata pointi tatu na hilo ndilo pekee analoliwaza kwasasa.

"Tumefurahi kushinda, haikuwa mechi rahisi ila ni kwasababu timu kwa ujumla ilicheza vizuri na tulitumia vizuri nafasi tulizotengeneza,'' alisema Kiiza.

Kwa mabao hayo mawili Kiiza amefikisha mabao nane sawa na straika wa Stand United Elius Maguli na Donald Ngoma wa Yanga ambao wamecheza mechi nyingi zaidi ya yeye ambaye alikaa nje muda mrefu akiuguza majeraha ya nyama za paja.

Akizungumzia mashabiki wenye hofu na kiwango chake na mipango yake juu ya kuchukua tuzo ya Mfungaji Bora, Kiiza alisema kuwa watu wanaomjua vizuri hawaongei, yeye hataki kujibizana na wanaomponda kuwa ameisha kupitia vyombo vya habari bali kwa kutumia miguu yake huku akisisitiza hana mpango wa kuwa mfungaji bora na hajawahi kuwaza hilo, yeye anachowaza ni kuibeba Simba ifanye vema.

"Hao hawamjui Kiiza, mimi ni yule yule na bado nina uwezo wa kufanya makubwa zaidi ya haya, miguu itaongea. Sijawahi kufikiria kuwa mfungaji bora na hayo si malengo yangu, mimi nataka kuisaidia Simba ibebe ubingwa bila kujali nani anafunga mabao," alisema Kiiza.

Simba inaenda mapumziko na pointi zake 21  ikiwa nafasi ya nne nyuma ya Yanga inayoongoza ligi kwa pointi 23, ikifuatiwa na Azam ikiwa na pointi 22 wakati Mtibwa wanashika nafasi ya tatu kwa kukusanya pointi 22.

Post a Comment

 
Top