BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda
TIMU ya taifa Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars' imeondolewa kwenye michuano ya Chalenji kwa changamoto ya mikwaju ya penati katika mchezo dhidi ya wenyeji Ethiopia.

Hadi dakika 90 za mchezo huo wa robo fainali zinamalizika, timu hizo zilitoshana nguvu kwa kufungana bao 1-1 hivyo kupelekea mechi hiyo kuingia katika hatua ya matuta ambapo Stars ilifungwa penati 4-3 na kufungashishiwa virago na kwa jumla ya mabao 5-4.


Stars ndio waliokuwa wa kwanza kutikisa nyavu kwa bao la John Bocco aliyefunga kwa kichwa katika dakika ya 24 ya mchezo. Bao hilo liliwapeleka Stars mapumziko wakiwa kifua mbele.

Katika dakika ya 55, beki kisiki Shomari Kapombe alimfanyia madhambi Mohamed Nasser wa Ethiopia kwenye eneo la penati hivyo kupelekea mwamuzi kuizawadia Ethiopia mkwaju wa penati ambao uliwekwa kimiani na Gathuoch Panom katika dakika ya 57.

Katika hatua ya matuta Ethiopia walipata penati nne huku Tanzania wakiambulia tatu tu.
Kapombe na Jonas Mkude walikosa penati huku Himid Mao, Bocco na Hassan Kessy wakiifungia Stars. Kwa upande wa Ethiopia wachezaji wote wanne waliopiga penati walifunga ambao ni Panom, Nasser, Aschalew Tamene na Behailu Girma.

Post a Comment

 
Top