BOIPLUS SPORTS BLOG

KIKOSI cha timu ya Taifa Tanzania Bara  'Kilimanjaro Stars' kimeendelea kutisha kwenye michuano ya Chalenji baada ya leo kuibamiza Rwanda mabao 2-1.

Kikosi hicho kilicho chini ya kocha Abdallah Kibadeni kilianza kupata bao lao la kwanza dakika ya 22 mfungaji akiwa ni kiungo, Said Ndemla dakika mbili baada ya kiungo wa Rwanda Jean Mugiraneza 'Migi' kuonyeshwa kadi ya njano kwa kufanya madhambi.


Stars waliendelea kuonyesha kandanda safi huku wakitafuta mabao ya kuongeza lakini hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika bado matokeo yalibaki kuwa ni bao 1-0 huku ikishuhudiwa Shomari Kapombe akionyeshwa kadi ya njano sekunde chache kabla ya timu hizo kwenda mapumziko.

Kipindi cha pili kilianza kwa kila timu kucheza mpira wa kutulia na kutafuta mabao lakini walikuwa Stars tena ndio waliofanikiwa kupata bao safari mfungaji akiwa ni kiungo, Simon Msuva.

Huku ikionekana kuwa mechi hiyo ingeisha kwa Stars kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, nyota wa Rwanda, Tuyisenge aliipatia timu yake bao la kufutia machozi katika dakika ya 89 ya mchezo. Kwa matokeo hayo Stars imefuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo kwa kufikisha pointi sita na mabao sita ya kufunga huku ikiwa imeruhusu bao moja tu.

Katika mechi ya awali, Zanzibar Heroes ilipata kipigo cha mabao 4-0 na Uganda, hicho kikiwa ni kipigo cha pili baada ya kupoteza mechi ya awali kwa bao 1-0 ilipocheza na Burundi.

Mabao ya Uganda leo yalifungwa na Farouk Miya aliyetupia mawili, Erisa Ssekisambu na Denis Okoth.
Mechi hiyo ilishuhudiwa wacheza wawili wa Zanzibar Herous, Mudathir Yahya na Mwadin Allywakitolewa nje kwa kadi nyekundu.

Post a Comment

 
Top