BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally
MSHAMBULIAJI wa Simba, Raphael Paul Kiongera raia wa Kenya amesema kuwa hawezi kurudi Simba mpaka amaliziwe fedha zake za usajili na mshahara wa miezi miwili ambayo hajalipwa.

Simba ilimsajili Kiongera akitokea timu ya KCB ya Kenya ambayo imeshuka daraja msimu uliopita wa Ligi Kuu Kenya (KPL) kwa dola 20,000 ambapo amedai kuwa viongozi wa Simba walimpa nusu ya fedha hiyo ambayo ni dola 10,000 na kubaki nusu ambayo hajamaliziwa mpaka sasa.


Kiongera aliichezea Simba mechi moja pekee ya Ligi Kuu Bara msimu uliopita dhidi ya Coastal Union ambayo aliingia akitokea benchi napo hakumaliza mechi hiyo kwani aliumia goti.

Hata hivyo, mwishoni mwa mwaka jana Simba iliamua kumpeleka Kiongera nchini India kwa ajili ya upasuaji wa goti hilo kwa gharama ya Sh 15 milioni na aliporejea nchini alikwenda kwao kwa ajili ya mapumziko na ndipo alijiunga na KCB kwa mkopo.

Kiongera alisema kuwa makubaliano ya mkataba wao alipokuwa KCB ni kwamba Simba ilitakiwa kumlipa nusu mshahara ambapo nusu nyingine ilikuwa inalipwa na KCB. Ikumbukwe kuwa mshahara wa Kiongera ni dola 1,500 kwa mwezi hivyo timu hizo zilikuwa zinatoa dola 750 kila moja.

''Siji huko kwani sijalipwa fedha yangu ya usajili, nilipewa nusu na bado nusu hata mshahara sijalipwa wa mwezi Juni na huu wa Novemba, naweza kuja kama watanilipa fedha zangu,'' alisema Kiongera.

Akiwa na KCB mshambuliaji aliwahi kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa mwezi Agosti katika ligi ya Kenya na amemaliza msimu akiwa ameifungia timu hiyo mabao 11 japokuwa alianzia katikati.

Alipotafutwa Rais wa Simba, Evans Aveva ili kutoa ufafanuzi juu ya madai hayo ya Kiongera, hakupatikana kwa vile mara zote alipopigiwa simu haikupokelewa.

Post a Comment

 
Top