BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda
UKIACHANA na siku ambayo nilitangazwa kimakosa kuwa nimeshinda Sh. 100 Milioni kwenye Bahati Nasibu, siku nyingine niliyopokea simu na ujumbe wa maandishi mara nyingi zaidi ni jana. Zaidi ya asilimia 80 ya simu hizo zilikuwa zinaulizia jambo moja tu "mechi ya Stars na Algeria itachezwa saa ngapi na itaonyeshwa na kituo gani cha Televisheni?".


Sikuacha kujibu hata ujumbe mmoja na kwangu hii ilikuwa ni furaha kubwa kwavile inaonyesha ni kwa kiasi gani Watanzania wameanza tena kuipenda na kuifuatilia timu yao ya Taifa tangu walipofanya hivyo kwa kiwango kikubwa wakati ikifundishwa na Mbrazili Marcio Maximo.


Kampeni kadhaa zilifanyika katika kuhakikisha Algeria inang'oka lakini kiukweli hapa tunapaswa kukiri tu tulichelewa kuiandalia mauaji Algeria ambayo yenyewe ilijiandaa kwa miongo kadhaa kuwa kama ilivyo sasa, kuitoa ilikuwa ni ndoto tu. Lakini pia maamuzi ya mwalimu Charles Mkwasa katika mechi ya jana yalionekana wazi kuwa yalitokana na kelele zilizopigwa na mashabiki baada ya mchezo wa kwanza uliopigwa kwenye dimba la Taifa jijini Dar Es Salaam.
Mechi hiyo ilimalizika kwa Stars kulala kwa mabao 7-0 hivyo kuondolewa kwenye mashindano hayo ya kuwania kufuzu kushiriki Kombe la Dunia 2018 kwa jumla ya mabao 9-2


NDEMLA, NGASSA JUKWAANI
Kitendo cha kuwaweka jukwani viungo Said Ndemla na Mrisho Ngassa kilionekana wazi kuwa ni cha kuwaridhisha mashabiki waliopiga kelele kuwa mabadiliko yaliyofanywa na Kocha Mkwasa ya kuwaingiza uwanjani badala ya Elius Maguli na Mudathir Yahya yalichangia Stars kutoa sare kwenye uwanja wa nyumbani.

Hii haikuwa sahihi, ni kweli mabadiliko hayo yalipunguza nguvu ya timu lakini kiufundi bado hakuwa na sababu ya kuwatupa jukwaani. Makosa yalikuwa ni ya Mkwasa mwenyewe kuingiza watu wanaowaza kushambulia zaidi badala ya kuingiza wakabaji ili kulinda ushindi wa mabao mawili. Hapa labda yeye mwenyewe ndio alipaswa kwenda jukwaani.


VIUNGO WAWILI WA KATI DHIDI YA ALGERIA?
Nilistaajabu tangu mchezo wa kwanza na sikuelewa kwanini mwalimu aliamua kuwatumia viungo wawili pekee, Himid Mao na Mudathir. Katika mchezo wa jana nilidhani angetumia winga mmoja Thomas Ulimwengu na kumpumzisha Farid Mussa huku kati akiweka viungo watatu ambao wangeweza kuwa Himid, Mudathir na Telela. Lakini kitendo cha mwalimu kupanga kikosi kile kile ndio kilinivuruga zaidi. Ina maana hakuwaogopa Algeria hata kidogo?

Ni wazi mechi ya jana ilikuwa kubwa sana kwa Farid Mussa ambaye hatukuona kabisa makeke yake, waarabu walifanikiwa kumficha kinda huyo ambaye nilitarajia mwalimu angemuanzisha bechi kupisha uwepo wa viungo watatu katikati ili kujaribu kuzuia mipango ya waarabu. Unapangaje watu watatu mbele ambao wote si wazuri katika kukaba?, Samatta, Ulimwengu na Farid si watu wa kuwategemea sana kwenye ukabaji ingawa angalau kidogo jana Samatta alionekana mara kadhaa akishuka kusaidia. Hapa Mkwasa alijiua mwenyewe.


KADI YA MUDATHIR ILIONEKANA MAPEMA SANA 
Tangu mwanzoni mwa mchezo Mudathir alionekana kupaniki huku akicheza rafu hata zisizokuwa na umuhimu, nilitarajia baada ya kupewa kadi ya njano ya kwanza basi mwalimu angeamua kumuokoa yeye na timu kwa kumtoa na nafasi yake kuchukuliwa na kiungo mwingine kati ya Telela na Jonas Mkude ambao walikuwa benchi. 

Naamini mwalimu aliliwaza hili jambo lakini kiukweli jana alikuwa ni kama mtu aliyeathirika kisaikolojia kwenye suala la kufanya mabadiliko, hapa mwalimu aliamua kuficha vyeti vyake na kutumia kelele za mashabiki akihofia kucheza kamali ya kumtoa Mudathir kama alivyofanya katika mechi ya awali. Matokeo yake ni kuibebesha timu mzigo mzito mara mbili. Kadi ya Mudathir ilichangia mabao kadhaa kwavile timu ilizidiwa mara dufu.

TUNAHITAJI WACHEZAJI BORA WANAOCHEZA NJE, SIO BORA WANACHEZA NJE
Ukizungumza na Samatta au Ulimwengu watakuambia ili Stars ifanye vizuri tunahitaji wachezaji wengi waende kucheza nje na kupata uzoefu zaidi. Nawakubalia kwa asilimia 50 huku 50 zingine zikibaki kwenye hofu yangu juu ya viwango vya wachezaji hao.

Ni kweli tunawahitaji wachezaji wa aina hii lakini ni lazima tukubali kuwa mwalimu anapaswa kuwaita wale tu walioonyesha uwezo. Wiki mbili zilizopita nilifika jijini Ndola, Zambia na kumshuhudia Juma Luizio, mshambuliaji wa zamani wa Mtibwa anayekipiga na Zesco ya nchini humo akicheza mechi. Alinikosha sana kwa uwezo wake na hata nilipozungumza na kocha wake alikiri kuwa hiyo ni hazina yao. 

Juma Luizio


Nilishangaa kuona mshambuliaji huyu aliyefunga mabao sita kwenye ligu huku akiwa amekosa mechi 11 kutokana na majeruhi hajaitwa timu ya taifa na badala yake akaitwa Ngassa ambaye bado hajafanya vizuri sana huko Afrika ya Kusini anakocheza. Na hata kwenye mchezo wa awali bado Ngassa hakuonyesha uwezo mkubwa kwenye dakika zaidi ya 20 alizopewa. 

TULIOTA MCHANA KUITOA ALGERIA, ILA 9-2 NI NYINGI MNO
Mawazo ya kuitoa Algeria inayoshika nafasi ya pili kwa ubora Afrika huku ikiwa na utajiri wa wachezaji wengi wanaocheza barani Ulaya yalikuwa ni mawazo ya kuishi kwa matumaini tu. Tunaweza kufanya hivyo baada ya kuandaa mkakati wa miaka isiyopungua mitano. Algeria wapo kilomita nyingi sana kutoka tulipo, ili kuwatoa unahitaji bahati ya kiwango cha juu mno.

Leo Azam inayoongoza ligi kuu ya Vodacom na Yanga inayoshika nafasi ya pili zina wachezaji wanne kila moja kwenye kikosi ya cha kwanza cha Stars. USM Alger iliyocheza fainali ya ligi ya Mabingwa Afrika haina mchezaji hata mmoja timu ya taifa ya Algeria. Tafakari, chukua hatua.

Post a Comment

 
Top