BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda, Ndola
STRAIKA wa zamani wa Mtibwa Sugar, Juma Luizio ameweka wazi kuwa hataongeza mkataba mwingine na timu yake ya sasa, ZESCO ya Zambia na kwamba mipango yake ni kwenda kucheza nchini Afrika Kusini au barani Ulaya.


Kauli hiyo aliitoa jana Alhamisi wakati wa mahojiano maalumu na BOIPLUS yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa jijini Ndola, kuwa maisha ya Zesco ni mazuri ukilinganisha na ya Mtibwa Sugar lakini hana mpango wa kuendelea kuishi hapo huku akieleza kuwa wachezaji wengi hapa wanaonekana wanapenda starehe.

Luizio alisema kuwa japokuwa kiasi cha fedha alicholipwa wakati wanamsajili pamoja na mshahara mnono ikiwemo posho nzuri na programu zao kuwa nzuri lakini anapaswa kuangalia mbele zaidi kwani mpira ndiyo ajira yake na tayari mawazo yake yapo sehemu nyingine.

"Malengo yangu ni kuondoka hapa mara mkataba wangu utakapomalizika, nataka nikacheze Afrika Kusini au Ulaya. Hapa wanalipa vizuri lakini huwa nakumbana na baadhi ya changamoto ndogo ndogo kama wachezaji wengi wanapenda kulewa ingawa hainisumbui sana," alisema Luizio.

Luizio ameisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Zambia ikiwa na pointi 64 ambapo yeye amefunga mabao sita huku akiwa amekosa mechi 11 ambazo hakucheza kutokana na kusumbuliwa na majeraha.

Zesco ilimsajili Luizio mwaka jana mkataba wa miaka mitatu kwa Sh 60 milioni, Mtibwa Sugar wao walilipwa Sh 70 milioni ambazo zilikuwa ni kwa ajili ya kuvunja mkataba, analipwa mshahara wa Sh 3 milioni ambapo kila timu yake inapocheza na kushindwa wanalipwa bonasi ya Sh 600,000 kila mchezaji.

Post a Comment

 
Top