BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Akram Msangi 'Mido'
WINGA Brain Majwega raia wa Uganda kwa sasa anafanya mazoezi na Simba kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kulinda kiwango chake ingawa BOIPLUS inafahamu kwamba Simba wanataka kumsajili mchezaji huyo ambaye alikuwa akikipiga Azam FC matajiri wa Ligi Kuu Bara.

Majwega hayupo na Azam tangu msimu uliopita ambapo habari za awali zilisema kuwa Kocha wa Wanalambalamba hao Stewart Hall hakukubaliana na kiwango cha winga huyo na kutaka kumtema lakini sasa iko tofauti kidogo.


Baada ya Majwega kukubaliwa kufanya mazoezi na Simba ambao wameonyesha nia ya kumsajili na wanasikilizia tu Shirikisho la Soka nchini (TFF) litakavyoamua katika kesi iliyopo kwenye shirikisho hilo kati ya Azam na Majwega ambayo ni kesi ya madai.

Azam wameibuka na kutangaza kuwa Majwega ni mchezaji wao halali na walishindwa kumlipa fedha zake kwasababu aliondoka kambini pasipo ruhusa hivyo walishindwa jinsi ya kumlipa.  BOIPLUS imefanya mahojiano na winga huyo ambapo ameelezea mambo mbalimbali katika soka lake.

TANGU AONDOKE AZAM
Majwega ameweka wazi kile alichoambiwa na viongozi wake wa Azam ambacho kwa maelezo yake ni kama alitelekezwa.

''Azam waliniambia niende KCC ya Uganda kwa mkopo lakini cha kushangaza nilivyofika huko viongozi wa KCC waliniambia hawajui chochote na hawana taarifa zangu nilimpigia simu Saady Kawemba hakuweza kupokea simu yangu ilikuwa inaita mpaka inakata wakati mwingine nikipiga anazima simu kabisa niliamua kufanya mazoezi mwenyewe tu kwa kipindi chote ambacho nilikua sina timu.''Mimi ni mchezaji na mpira ni kazi yangu naendesha maisha yangu kwa kutegemea mpira kama sijacheza unafikiri nitaendeshaje maisha yangu?
Ona sasa sijaitwa hata timu yangu ya Taifa naumia sana bila kucheza kiwango changu kinashuka,'' anasema Majwega ambaye amegoma katakata kurudi kuichezea Azam Fc

UJIO WAKE SIMBA
Kila mtu ana chaguo lake lakini Majwega anaelezea zaidi ujio wake ndani ya Wekundu wa Msimbazi hao huku akitanguliza kicheko huku akielezea kwanini amechagua kufanya mazoezi Simba pekee.

''Mimi sijasajiliwa Simba nimeandika barua TFF wanisaidie swala langu na Azam nipate haki zangu na waniache niwe huru kwanza naweza kucheza,  hapa Simba niliomba nifanye mazoezi kama mambo yakienda vizuri naweza kusaini Simba.''Niliamua kuomba Simba kwasababu Simba ni timu kubwa na kuna watu wazuri na marafiki zangu wapo Simba. Na ninapenda kucheza tanzania kwasababu ligi ya Tanzania ina ushindani mkubwa,'' anasema Majwega ambaye anajiamini kuwa akisaini Simba nafasi yake kikosini ipo wazi.

MTAZAMO WAKE SIMBA
''Maisha ya Simba ni mazuri wachezaji wanapendana, mashabiki wanapenda timu yao kila kitu Simba ni kizuri. 
Nawaahidi mambo mazuri mashabiki na wanachama wa Simba na waniombee Mungu swala langu na Azam liishe salama niwafanyie kazi,'' anaeleza Majwega

HATISHWI NA YANGA
Ligi Kuu ya Vodacom mechi kubwa sana na yenye upinzani mkubwa lakini Majwega anasema endapo atafanikiwa kutua Simba hana wasiwasi juu ya Yanga hasa pale watakapokutana.''Nimejipanga tu vizuri kwasababu mimi ni mchezaji na mchezaji unatakiwa ujiamini kwa njia yoyote hivyo hilo halina tatizo kwangu,'' anasema na kuongeza

''Sijaja Simba kwa ushawishi wa mtu bali nimekuja baada ya kukubaliwa kufanya mazoezi na kuna rafiki zangu ndani ya Simba ambao wanacheza,''

CHANGAMOTO
''Changamoto katika soka zipo nyingi tu lakini kubwa ni pale kiongozi anakufuata na kukuambia kocha hakutaki hivyo unapelekwa kwa mkopo timu nyingine bila mkataba wowote uliofanywa baina ya timu husika, huwa inaumiza sana.

''Azam wanataka tu kuniharibia wanasema mimi mchezaji wao sawa mbona hawanipi mshahara miezi sita nadai na hawanipi ushirikiano?
Kawemba aliniambia kocha amesema sina nafasi kwenye timu yake basi 
waniache nicheze mpira,'' anasema kwa masikitiko.

 AISHAURI SIMBA
''Kwanza nianze na wachezaji wajitume zaidi ili kuwapa moyo mashabiki wao ambao wana wasapoti kila mahali, viongozi wawe karibu na wachezaji waweze kuyajua matatizo yao na kuyatatua. Mashabiki pia  wasichoke kuisapoti timu, Mungu ni mwema mambo yatakuwa mazuri,''.SOKA LA BONGO
''Soka la Tanzania ni zuri na ushindani ni mkubwa vipaji ni vingi lakini vinapotea kwasababu viongozi hawako makini. Mfano mimi nikikaa na kushindwa kucheza mpira kiwango kitashuka nitapotea kwenye ramani ya soka.

''Viongozi wanadhulumu haki za wachezaji. Mimi nataka hata tukikubaliana mshahara wa Sh 2,000 basi nipewe hiyo fedha yangu sasa hapa unakubaliana Sh 2,000 unapewa 500 hiyo ni nini? Naweza kusema ni dhuluma kubwa,'' anasema Majwega

Endapo Simba itafanikiwa kumsajili Majwega basi ataungana na wenzake wawili raia wa Uganda ambao ni Hamisi Kiiza na Juuko Murshid.

Post a Comment

 
Top