BOIPLUS SPORTS BLOG

SHIRIKISHO la Soka nchini (TFF) limemaliza utata uliokuwepo katika ya klabu ya Azam na winga Brian Majwega na sasa mchezaji huyo atasaini mkataba rasmi wa kuichezea Simba ambayo tayari alianza kufanya nayo mazoezi.

Azam na Majwega walikuwa na matatizo ya kimkataba ambapo mchezaji huyo aliondoka kwenye klabu hiyo baada ya kocha wao, Stewart Hall kutoridhishwa na kiwango chake bila hata kumpatia haki zake ikiwemo kutolipwa mshahara wake.



Kesi hiyo ilipelekwa TFF ambapo Majwega  pia aliomba kufanya mazoezi na Simba huku akiwa anasubiri hatima ya kesi hiyo na kusisitiza kuwa hata iweje asingeweza kurudi kuichezea Azam ambayo ilikuwa inadai kuwa bado winga huyo ni mali yao halali.

Chanzo cha habari kutoka TFF kimeiambia BOIPLUS kuwa tayari uamuzi umefanywa lakini bado hawajatangaza rasmi ila Majwega yupo huru kusaini Simba.

''Nafikiri hata kesho au siku yoyote taarifa itatolewa rasmi na TFF kwa kesi ya msingi imeisha na Majwega anaruhusiwa kusajiliwa timu yoyote kwa mujibu wa kanuni za usajili wa ligi yetu,'' alisema kiongozi huyo wa TFF.

Hiyo ni taarifa njema kwa Simba ambao wanahitaji huduma ya Majwega kwa muda mrefu pasipo mafanikio na sasa atafikisha idadi ya wachezaji sita wa kigeni ndani ya Wekundu hao wa Msimbazi, wengine ni Hamisi Kiiza, Juuko Murshid, Justice Majabvi, Emery Nimubona na Vincent Angban na hivyo imebaki nafasi moja kujaza kufikisha idadi saba ya wachezaji wa kigeni.

Post a Comment

 
Top