BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Karim Boimanda, Lubumbashi
UKIPITA mitaa ya Jiji la Dar es Salaam siku ambayo Yanga inavaana na  Etoile Du Sahel katika mechi ya Kombe la CAF basi utaona jezi nyingi za kijani na njano lakini ni lazima utakutana na jezi nyekundu za waarabu hao ambazo nyingi zinakuwa zimevaliwa na mashabiki wanaoaminika kuwa ni Simba. Hali kadhalika siku Simba inapambana na FC Libolo ya Angola pale Uwanja wa Taifa basi utakutana na jezi nyingi zenye rangi nyekundu na nyeupe ila usishangae kukutana na jezi za kutosha tu za Libolo, hawa waliovaa si tu mashabiki wa Libolo, bali ni mashabiki wanaoaminika kuwa ni Yanga.

Hali ni tofauti kabisa na hapa jijini Lubumbashi, rangi pekee zinazoonekana mitaani ni nyeupe na nyeusi ambazo zinatumiwa na klabu tajiri ya TP Mazembe Englebert iliyoanzishwa mwaka 1939 miaka minne baada ya Yanga kuanzishwa na mitatu baada ya Simba kuanzishwa. Jezi nyekundu za USM Alger zimevaliwa na viongozi, wachezaji na mashabiki wachache wa timu hiyo ambao unaweza kuwatofautisha kabisa na wa hapa Lubumbashi kwavile wengi wao wanaonekana wana asili ya kiarabu.


Hii ni makala ambayo BOIPLUS imeelezea  maandalizi ya timu hiyo inayomilikiwa na milionea Moise Katumbi Chapwe anayetajwa sana na wananchi kuwa ndiye Rais ajaye wa DR Congo.

WACHEZAJI 'FULL' MZUKA
Huenda ni kwasababu ya ushindi wa mabao 2-1 walioupata wiki moja iliyopita jijini Algers au ni maandalizi kabambe waliyoyapata mara baada ya kurejea hapa jijini Lubumbashi. Lakini ari inayoonyeshwa na wachezaji wa Mazembe ni ya hali ya juu. 

Akizungumza na BOIPLUS, kipa mkongwe wa timu hiyo Robert Kidiaba alisema kwa upande wao kila kitu kiko tayari na kilichobaki ni kuingia uwanjani na kuwapa furaha mashabiki wao.

"Si unaona wachezaji tulivyo na amani, hii inaonyesha hakuna kilichobaki, ni kuutafuta ushindi tu," alisema Kidiaba kipa mwenye makeke awapo uwanjani ila mpole nje ya uwanja.


Kwa upande wake straika tegemeo wa Mazembe na Taifa Stars, Mbwana Samatta 'Etoo wa Mbagala' alisema anajua mechi  itakuwa ngumu kwavile USMA wataingia kama mbogo aliyejeruhiwa wakitafuta bao la mapema kama walivyopata wao kule Algers ili kuwachanganya, ila wao wamejipanga kupambana na hali yoyote ile.

"Jamaa watakuja kwa kasi wakitamani kutushtukiza lakini sisi tumejiandaa kwa mtindo wowote wa mchezo, hakuna namna, mechi iwe 'fifty fity' (50% kwa 50%) au vinginevyo, mwisho wa siku tutawashambulia tu tuwafunge,'' alisema Samatta ambaye ameshapokea bendera yake ya Taifa aliyokuwa akiihitaji sana.

KOCHA YEYE ANAWAZA MABAO TU
Mfaransa Patrice Carteron kwa upande wake yeye alisema ameshamaliza maandalizi yote na anaamini ili kubeba kombe hili hapaswi kuitafuta sare, bali ushindi ambao utapatikana kwa kufunga mabao.


"Watu wanaizungumzia fainali hii kuwa imeshakufa, ni nyepesi kwetu kwavile tulishinda kule kwao, si kweli, ni ngumu na tunalazimika kushinda tu ili tubebe ubingwa.

"Na ili ushinde mechi ni lazima ufunge mabao, nimewaambia akina Samatta wafunge mabao mengi iwezekanavyo kwavile huko ndio kwenye ubingwa,''alisisitiza Carteron.

MOISE KATUMBI AAHIDI ZAWADI, AGOMA KUITAJA
Imezoeleka kila inapotokea mechi kubwa basi Katumbi huwaahidi madola wachezaji wake ili kuwapa motisha, safari hii kaja kivingine, amewaambia kuna zawadi kubwa imeandaliwa ila ni siri yake. 
Katumbi pia amewaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu yao kwavile anaamini ushindi upo mikononi mwa mashabiki hao huku akiwasihi kuepuka vurugu zozote.

"Zawadi ipo ila ni siri, hakuna anayejua zaidi yangu. Mashabiki waje kwa wingi uwanjani kuipa sapoti Mazembe huku wakizingatia asili yetu, sisi ni wastaarabu, hata mtu akitushinda nyumbani haturushi mawe, tunakubali matokeo,'' alisema Katumbi.

KILA KONA NI SAMATTA

Ukitaka mambo yakuendee sawa kwenye Taxi, Hotelini, Bar au hata mazoezini, we sema tu 'mimi natoka Tanzania kwa akina Samatta' hapo utakuwa umejihakikishia huduma bora. 
Samatta amefanikiwa kuteka nyoyo za wakongo kiasi kwamba kila shabiki unayemuuliza anatarajia nani atampa furaha kwenye fainali hii basi atakuambia Samatta.

"Ally (Samatta) ni hatari sana, atafunga tu sina hofu, na yule Ulimwengu ana nguvu, atasababisha mabao mengi,'' alisema  kwa kujiamini shabiki mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Heritier.


Akizungumzia hali hiyo Samatta alisema ni changamoto kwake ila sasa ameshazoea.

"Nimeishazoea sasa kaka, namuomba Mungu tu aniwezeshe kuwafanyia kile wanachokitarajia,'' alisema Samatta ambaye sasa anazungumza kifaransa kama kazaliwa Lubumbashi.

MASHABIKI WAFANYA USAFI UWANJANI
Katika hali ya kustaajabisha, licha ya Uwanja wa Mazembe kuwa na wafanyakazi wengi, mashabiki wa timu hiyo waliamua kuwapora fagio wafanyakazi hao na kuanza kufagia barabara zinazoingia uwanjani hapo huku wakiimba 'sebene' za kuipamba timu yao.


Ndani ya Uwanja BOIPLUS iliwashuhudia akina mama wengi ambao ni wafanyakazi wa Uwanja wakiwa na vitambaa na ndoo za maji wakifuta viti vya uwanja huo. Cha kufurahisha ni kwamba licha ya kulipwa fedha, bado wana mapenzi na timu yao. Wanafanya kazi zao huku wakiimba Mazembe kwa hisia kali.

KILA TELEVISHENI NI MAZEMBE TU
Kama hutaki kuona habari za Mazembe basi wewe zima TV yako ulale tu, kwa maana kila kituo utakachofungulia utakuta aidha nyimbo za kumsifu Katumbi na Mazembe yake au 'highlights' za mechi za zamani za Mazembe.

Kama unapenda muziki basi utashtuka unaimba tu nyimbo za Mazembe bila kujijua kwa maana ndizo pekee zinazosikika sana.

Kwenye suala la maandalizi hakuna hofu yoyote kusema Mazembe wamejitahidi kwa asilimia nyingi, je uwanjani hali itakuaje?

Tembelea BOIPLUS kila wakati utafahamu kila kinachojiri hapa Lubumbashi katika fainali hii itakayopigwa kuanzia saa 9:30 alasiri kwa saa huku sawa na saa 10:30 kwa saa za Afrika Mashariki.Post a Comment

 
Top