BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally, Blida, Algeria
MATOKEO ya sare ya mabao 2-2 ni kama yameharibu rekodi ya straika wa Taifa Stars na TP Mazembe, Mbwana Samatta ambaye amesema kuwa endapo wangetoka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Algeria yangempandisha chati zaidi kwenye mbio za kuwania tuzo ya Mchezaji Bora anayecheza klabu za ndani ya Afrika.

Samatta ambaye ni Mfungaji Bora wa michuano ya Mabingwa wa Afrika amesema kuwa hii ingekuwa ni historia kubwa kwake pamoja na Tanzania kwa kuifunga Algeria ambayo ni miongoni mwa timu bora Afrika kwenye viwango vya Fifa.


"Ingekuwa ni mafanikio makubwa kwangu, kutwaa ubingwa wa Afrika nikiwa na TP Mazembe na kuifunga Algeria, lakini imekuwa tofauti,  nilipambana vya kutosha ila matokeo yake tuliishia kutoka sare ingawa bado tuna nafasi ya kushinda kesho," alisema Samatta.

Katika hatua nyingine, Samatta alijikuta yupo katika wakati mgumu mara baada ya kushuka uwanja wa Ndege ambapo mashabiki wa soka wa Algeria walikusanyika wakimsubiri mchezaji huyo wakitaka kupiga naye picha.

Samatta alijitahidi kuwakwepa ikiwa ni pamoja na kuwakimbia lakini haikusaidia na baadaye kulazimika kupiga nao picha ili kumalizana nao huku mashabiki hao wakitamka wazi kuwa walikuwa wanamsubiri Samatta.


Kiongozi wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Msafiri Mgoyi alilazimika kuingilia kati kwa kuwataka mashabiki hao waache kumzonga Samatta na kumuacha aungane na wenzake kwani alikuwa amechoka na safari hiyo.

Stars inacheza kesho mechi ya marudiano ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2018 ambapo inashika nafasi ya 135 kwenye viwango vya FIFA wakati Algeria wao wanashika nafasi ya 25. Na ili Stars isonge mbele inahitaji ushindi wa bao 1-0 ama sare ya bao 3-3.

Post a Comment

 
Top