BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally
STRAIKA wa Yanga, Matheo Anthony mpaka sasa amecheza dakika 90 kwa mechi mbili ndani ya kikosi hicho lakini amesema kuwa anamshukuru Kocha wake Hans Pluijm ameanza kuona umuhimu wake.

Mechi ya kwanza aliingia kuchukuwa nafasi ya Amissi Tambwe timu hiyo ilipocheza na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro na nyingine alichukuwa nafasi ya Donald Ngoma walipocheza na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Alli Hassan Mwinyi, Tabora.

Matheo (kushoto) alipokuwa akiichezea KMKM ya visiwani Zanzibar


Akizungumza na BOIPLUS, Matheo alisema kuwa anaamini atapata nafasi zaidi kwenye kikosi cha Pluijm kwani isingekuwa rahisi kwake kufika na kuanza kikosi cha kwanza moja kwa moja.

''Nafurahi kocha ameanza kuona uwezi wangu na njia pekee ya kumshawishi zaidi ni kujituma mazoezini. Binafsi huwa napenda kumwachia kocha aamue kwani yeye ndiye mtu wa mwisho kwenye timu kazi yangu ni kujituma zaidi.

''Mimi nimeingia Yanga kipindi hiki isingekuwa rahisi kuniamini moja kwa moja kwani kuna wengine nimewakuta kwenye ligi hii ya Bara lakini bado hawajapewa nafasi ya kucheza ndani ya timu zao. Hivyo mechi mbili nilizopewa ni mwanzo mzuri,'' alisema Matheo.

Matheo amesajiliwa msimu huu akitokea KMKM ya Zanzibar ambayo pia aliichezea michuano ya Kombe la Kagame pekee bila hata kuonja Ligi Kuu ya Zanzibar akitokea timu ya daraja la chini.

Post a Comment

 
Top