BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Sheila Ally
ALIYEKUWA Kocha Msaidizi wa Simba, Seleman Matola amejiuzulu juzi usiku lakini jana vigogo wa Simba walikuwa na mtihani mgumu wa kusaka mbadala wake ambaye ufumbuzi wake bado haujapatikana.

Matola ameikacha Simba kwa kile alichokieleza kuwa hawezi kufanya kazi na kocha mkuu Dylan Kerr kwani ni mbishi na asiyehitaji ushauri kutoka kwa wenzake mpaka kufikia hatua ya kujibizana mbele ya wachezaji wao jambo ambalo si zuri.


Jana baadhi ya viongozi wa Simba walikuwa na vikao vya mara kwa mara kujadili juu ya mustakabali mzima wa kumpata kocha atakayesaidiana na Kerr ambaye pia baadhi ya viongozi hawamtaki kuiongoza Simba. Matola atakuwa ni kocha wa pili kutofautiana na Kerr ambapo mara ya kwanza alikwaruzana na kocha wa viungo Dusan Momcilovic.

Baada ya kukwaruzana na Dusan, Kerr aliona njia mbadala ni kumwondoa ambapo viongozi wa Simba walimsikiliza na kuamua kumfungashia virago huku wakiwa bado wanahitaji huduma ya kocha huyo wa viungo.


Chanzo cha ndani kutoka Simba kinasema kuwa baadhi ya viongozi wa juu kutoka ndani ya Kundi la Friends of Simba wamekuwa wakimuunga mkono Matola na kumpinga vikali Kerr kitu ambacho kimeleta msuguano kwa wanachama hao na kushindwa kuwa na maamuzi sahihi na ya pamoja.

''Matola amejiuzulu lakini wengine hawajakubali kwa moyo mmoja ambao ndio hao wasiomtaka Kerr hivyo siku ya jana wamekuwa wakijadiliana ili kujua nani atarithi nafasi ya Matola na Kerr itakuwaje,'' alisema kiongozi huyo.

Hata hivyo Rais wa Simba, Evans Aveva amesema kuwa ''Ni kweli tupo katika mchakato wa kumpata kocha msaidizi tunaangalia kote kote ndani na nje ya nchi. Kama tutapata hapa hapa sawa kama itakuwa nje ya nchi napo sawa. Mpaka wiki ijayo tutakuwa tumejua nani atamrithi Matola ila kiukweli ametuvuruga,''.

Kuhusu usajili katika dirisha dogo amesema ''Wiki ijayo ndiyo kila kitu kitajulikana kuhusu usajili na mambo mengine hivyo tunajipanga ili tukutane mechi ya Stars ikipita tujue tunafanyaje,''.


Habari zaidi zinasema kuwa Simba walianza kufanya mazungumzo na kocha Cedrick Kaze wa Burundi lakini bado kuna ugumu kutokana na kocha huyo kuwa na CV ya maana kuliko Kerr na inadaiwa kuwa amewaeleza wazi kuwa wakihitaji huduma yake basi awe kocha mkuu. Kaze ana leseni A ya ukocha inayotambulika na Caf pamoja na Fifa.

Chaguo lingine kwa Simba upande wa kocha mzawa ni Bakari Shime wa Mgambo JKT lakini naye imeelezwa kuwa anamkataba na Shirikisho la Soka nchini (TFF) kwani ni kocha wa timu ya taifa ya vijana. Hivyo mpaka wiki ijayo wanachama wa Simba wataambiwa ukweli juu ya kocha atakayepatikana kama hao wote  itashindika.

Post a Comment

 
Top